Msajili wa Vyama vya siasa Jaji Fransis Mutungi wakati akizungumza na waandishi wa habari akitolea ufafanuzi kuhusu jitihada zinazofanyika za kuondosha mvutano unaojitokeza kati ya Polisi na Vyama vya siasa Nchini
****************
Vyama vya siasa Nchini vimetakiwa kuwa wavumilivu kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakumba katika siasa bali waendelee kulipenda taifa pamoja na kuwatii viongozi ili taifa liendelee kusonga mbele kimaendeleo.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Msajili wa Vyama vya siasa Jaji Fransis Mutungi wakati akizungumza na waandishi wa habari akitolea ufafanuzi kuhusu jitihada zinazofanyika za kuondosha mvutano unaojitokeza kati ya Polisi na Vyama vya siasa Nchini.
Jaji Mutungi amesema wamepanga kufanya mkutano wa kuwakutanisha Jeshi la Polisi na viongozi wakuu wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kuduma kwa lengo la kujadili na kuelimishana kuhusiana na mwenendo wa vyama vyao ili kuondoa mvutano unaojitokeza kati ya Polisi na baadhi ya vyama hivyo.
Aidha Jaji Mutungi amesema amewasiliana na IGP ili kuwakutanisha wadau hao kwani wanataka isifike mahala sio kila mkutano wanaotaka kufanya Polisi wamejaa hivyo lengo lao ni kuondoa taharuki hiyo.
Amesema siasa ya nchi haijafikia hatua ya taharuki hiyo bali ni suala la kueleweshana sambamba na kuwekana wazi ili kuweka bayana wanapopishana baina ya wadau hao.
“Sisi tunasema hakuna sintofahamu bali ni suala la kuwekana wazi na nadhani tunapozungumza jamii ni familia ya wanasiasa ni watu wazima watu wenye uchungu na nchi hivyo tunataka tuondoshe hicho kitu ambacho Polisi wanaona wanasiasa wanakosea hapa na wanasiasa wanaona Polisi wanakosea hapa hivi kwa nini tusikae meza moja kama tulivyokaa hapa tukaweka bayana wapi tunapishana’amesema Jaji Mutungi
Hata hivyo Msajili huyo wa vyama vya siasa amesema kikao hicho kitaleta mustakabali wa wanasiasa juu ya taifa lao ambalo kila siku linaimba kuhusiana na uzalendo.
Tangu ufanyike uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kumekuwa kukiibuka misigano baina ya baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani na jeshi la polisi ambalo kwa nyakati kadhaa limetajwa kuzuia baadhi ya matukio ya kisiasa ikiwemo mikutano ya ndani na makongamano kwasababu mbalimbali