Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi (aliyesimama) akiongea katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Tabora kilichofanyika juzi Mkoani hapa ili kupokea taarifa ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Mkoa huo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Balozi Dkt Batilda Salha Burian.
……………………………………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
WAJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuteua viongozi wenye weledi mkubwa wa kusimamia utekelezaji ilani ya uchaguzi.
Pongezi hizo zimetolewa juzi katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo Cha Utumishi wa Umma chini ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa Hassan Wakasuvi.
Katibu wa CCM wilaya ya Tabora Mjini Nicholous Malema alisema Viongozi walioteuliwa hivi karibuni na Mheshimiwa Rais Samia wanafanya kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji ilani ya uchaguzi ya chama kwa manufaa ya wananchi.
‘Tunampongeza sana Rais kwa kutengeneza safu ya kazi yenye weledi mkubwa, inayolenga kuharakisha maendeleo ya wananchi, Ma-RC, Ma-DC, Ma-DED na Viogozi wa Wizara kila siku wako kazini, kazi inaendelea vizuri’, alisema.
Aidha alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Mkoani humo Hassan Wakasuvi na Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa kazi nzuri ya kufuatilia kwa karibu zaidi miradi inayotekelezwa katika wilaya zote na kutoa maelekezo wanapobaini mapungufu.
Kwa upande wake Mwenyekiti Wakasuvi alizitaka halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha fedha zote zinazoletwa kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo zinatumika kwa kazi iliyokusudiwa na zisirudishwe hazina kuu kama mradi utakuwa haujakamilika.
Aidha alimwagiza Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian kuhakikisha halmashauri zote zinatumia mfumo wa kielektroniki (POS) kukusanya mapato katika maeneo yao ili kudhibiti upotevu na kuharakisha utekelezaji miradi.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui ambaye pia ni diwani wa Isila wilayani humo Said Ntahondi alisema halmashauri nyingi zina upungufu mkubwa wa mashine za POS hivyo kupelekea kushidwa kukusanya mapato mengi.
Aliomba serikali kuangalia uwezekanao wa kuziongezea halmashauri zote vifaa hivyo ili kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kuziwezesha kufikia malengo ya makusanyo waliyojiwekea.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora Ramadhani Kapela alisema wamefurahishwa na uamuzi wa Rais Samia kupeleka kiasi cha sh bil 1.5 katika kila jimbo kwa ajili ya kuboresha barabara za mjini na vijijini, alishauri madiwani na wabunge kukaa meza moja ili kubainisha barabara zitakazotengenezwa.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Sikonge Anna Chambala alielezea kufurahishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya 6 katika kumaliza kero za wananchi, alishauri suala la wakulima na wafugaji kupewa kipaumbele pia kwa kutengewa maeneo ya malisho ili kuboresha shughuli zao.
Akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali za wajumbe Mkuu wa Mkoa huo Balozi Batilda Burian alisema kuwa mashine za POS zina mchango mkubwa sana katika ukusanyaji mapato hivyo akabainisha kuwa juhudi za kupata mashine zaidi zinaendelea kufanyika.