*****************************
Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
WALIMU na wazazi wameaswa kushirikiana kuwasimamia wanafunzi wenye vipaji maalum ikiwa ni pamoja na wanaomudu masomo ya sayansi ,katika shule za msingi ili kufikia elimu ya sekondari na kukuza taaluma zao.
Aidha jamii imetakiwa kuunga mkono juhudi za serikali kutatua changamoto mbalimbali kwenye sekta ya elimu pasipo kuiachia pekee .
Akizungumza na walimu ,wageni, wanafunzi na viongozi mbalimbali kwenye mahafali ya shule ya msingi Chalinze Modern Islamic, kwa niaba ya mgeni rasmi mbunge wa Jimbo la Chalinze,Ridhiwan Kikwete ,mkuu wa sekondari Lugoba,Abdallah Sakasa alibainisha, elimu ndio nguzo kwa watoto wetu.
Alisema wanafunzi wanaofanya vyema shule za msingi wanapaswa kusimamiwa ili kuepuka na masuala yasiyofaa ambayo yanaweza kuwaharibia mwanzo wao mzuri waliouanza.
Hata hivyo ,Sakasa aliiasa jamii kushirikiana na serikali kuboresha na kutatua changamoto za kielimu ikiwemo majengo ya madarasa .
“Ridhiwani amewaomba wazazi kufanya jitihada ya Kujenga shule ya sekondari shule hapa ,ili kusogeza upatikanaji wa elimu ya sekondari karibu,na ameahidi kuchangia mifuko ya saruji 50 na kokoto Lori mbili “alifafanua.
Hata hivyo Sakasa alisema ,ofisi ya mbunge kwa kushirikiana na mamlaka nyingine watasimamia miradi ya maji inayoendelea ili shule ya Chalinze Modern Islamic iondokane na changamoto ya ukosefu wa maji ya uhakika.
Mkuu wa shule hiyo,Amran Bakari alieleza ,shule hiyo imeanzishwa mwaka 20, kwasasa kuna jumla ya wanafunzi 575 ambapo 272 Ni wanafunzi wa kiume na 301 wasichana.
Awali mkurugenzi wa Kimara Islamic center (KIC) inayosimamia Chalinze modern Islamic na Matangini Islamic sekondari,Abdul Kiriwe alifafanua ,shule hizo zinatoa elimu bora na kusimama maadili mema.
Aliwaomba wazazi, kuwaendeleza watoto hao elimu ya sekondari na kusimama kwenye maadili ya dini na kuwachunga ili wasipotee kitabia.
Kiriwe alisema,wamebeba dhamana ya kumsomesha mwanafunzi aliyetoa mada ya sayansi (Embryolohy),Ghania A’Aziz kuanzia kidato cha kwanza hadi Cha sita katika shule ya sekondari ya Matangini Islamic Kimara.
Nae kiongozi wa dini ,alhaj Hamis Nassor aliwaomba wazazi na walezi kuunga mkono ujenzi wa kuanzisha shule ya sekondari ilihali wanafunzi wanaoanzishiwa mwanzo mzuri shuleni hapo waendelee na sekondari katika shule hiyo.
Katika kuchangia ujenzi wa shule ya sekondari Chalinze Modern Islamic ,imepatikana milioni zaidi ya 11 .