***************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
NATARIA mtoto wa msanii maarufu wa bongofleva Ras Lion aliyeimba wimbo maarufu wa Shikamoo Bibi kwa ajili ya Rais Samia Suluhu Hassan, amewaacha midomo wazi na kuwafurahisha wananchi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakati wa kuwatumbuiza.
Msanii huyo aliimba wimbo huo wakati wananchi hao wakimsubiri Rais Samia ambaye ametembelea mji mdogo wa Mirerani kwa ajili ya kurekodi kipindi cha kutangaza kimataifa madini ya Tanzanite.
Wimbo wa shikamoo bibi alioimba msanii huyo Nataria mwenye umri wa miaka mitatu uliwafurahisha na kuwaacha hoi mamia ya watu waliohudhuria eneo hilo.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Philip Gekul, amempongeza msanii huyo chipukizi kwa kumtunza fedha wakati akiimba wimbo huo maarufu wa Shikamoo Bibi.
Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Bilionea Saniniu Laizer na Mkurugenzi wa Tanzanite Forever Ltd, Faisal Juma ni miongoni mwa watu maarufu waliojitokeza kumtunza msanii huyo.
Wabunge mbalimbali wa Mkoa wa Manyara, wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Mbunge wa Vijana Taifa kupitia Mkoa wa Manyara, Asia Halamga na Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Regina Ndege walimpongeza na kumtunza fedha msanii huyo.
Pia, Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Wakili msomi Edward Ole Lekaita Kisau, Mbunge wa Jimbo la Hanang’ mhandisi Samwel Hhayuma Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini Paul Zacharia Isaay na Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Maasay, walimtunza fedha msanii huyo.
Msanii maarufu Ras Lion amesema mtoto wake huyo amerekodi wimbo huo kwenye studio za Africanas Record kwa Manrick zilizopo Mji mdogo wa Mirerani.
“Ana umri wa miaka mitatu na miezi saba, anasoma chekechea kwenye shule ya awali na msingi Blue Tanzanite hapa Mji mdogo wa Mirerani,” amesema Ras Lion.