Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Dk.Philip Isdor Mpango (katikati) akikabidhiwa sehemu ya mchango wa rimu za Karatasi 1,500 kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa darasa la saba jijini Dodoma waliopo kwenye makambi ya kujindaa na mtihani wa taifa unaoanza wiki hii. Kutoka kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NMB – Dk.Edwin Mhede, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Tulia Ackson na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Dk.Philip Isdor Mpango (katikati) akikabidhiwa sehemu ya mchango wa taulo za kike kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa darasa la saba jijini Dodoma waliopo kwenye makambi ya kujindaa na mtihani wa taifa unaoanza wiki hii. Kutoka kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NMB – Dk.Edwin Mhede, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Tulia Ackson na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Dk.Philip Isdor Mpango akiwaongoza washiriki waliojitokeza katika Tamasha la Kivumbi na Jasho lililowashirikisha Benki ya NMB na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, jijini Dodoma. Walioongozana nae kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NMB – Dk.Edwin Mhede, Mwenyekiti wa Bunge Sport Club, Mhe. Abass Tarimba , Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Tulia Ackson, Mke wa Makamu wa Rais, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna akiteta jambo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Job Ndugai katika mchapalo ulioandaliwa kuhitimisha Tamasha la Kivumbi na Jasho jijini Dodoma.
******************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Phillip Isdor Mpango, amesifu malengo chanya ya Tamasha la NMB na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kufichua kuwa yamewavutia Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa.
Tamasha hilo lililotambulika kama ‘NMB Kivumbi na Jasho’, lilifanyika jijini Dodoma, likianza na Matembezi ya hisani kuanzia viwanja vya Bunge hadi viunga vya Chinangali Park, ambako Dk. Mpango aliyekuwa mgeni rasmi, alipokea mchango wa NMB wa kuboresha elimu jijini Dodoma wenye thamani ya Sh. Milioni 17 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthon Mtaka.
Tamasha la Kivumbi na jasho lilivuta hisia na kuhudhuriwa na wabunge wote walioongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania – Mhe.Tulia Akson, Mke wa Makamu wa Rais, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. George Simbachawene na Mawaziri mbalimbali.
Mchango huo uliotolewa na Benki ya NMB ni rimu za karatasi bunda 1,500 zenye thamani ya shilingi milioni 15 na taulo za kike zenye thamani ya shilingi milioni mbili maalumu kwaajili ya wanafunzi wa darasa la saba waliopo kwenye makambi wakijiandaa na mtihani wa darasa la saba.
Akizungumza kabla ya kumkabidhi mchango huo Dk. Mpango, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bi. Ruth Zaipuna alimueleza Makamu wa Rais kuwa Benki ya NMB imetumia Tamasha la NMB na Wabunge, kuzindua mpango endelevu wa kuchangia maendeeleo ya watanzania kwa kutazama mahitaji ya eneo husika ambapo michango hiyo itafanyika kila baada ya miezi mitatu. Licha ya tamasha hili kuanzia Dodoma, litasambaa kote nchini kwani NMB ina matawi nchini kote.
Kwa jiji la Dodoma, mpango huo umelenga kuchangia zaidi utatuzi wa changamoto za elimu, pamoja na ‘Mpango Mkakati’ wa kuligeuza jiji la Dodoma kuwa la kijani kupitia upandaji miti na utunzaji mazingira.
“Leo kupitia tamasha hili, tunazindua program hiyo endelevu, itakayo kuwa inafuata kalenda ya vikao vya Bunge hapa Dodoma, ili kila litakapofanyika tamasha hilo, wabunge wote wawe sehemu ya washiriki. Kila tutapokutana hapa tutakuwa na kauli mbiu maalum inayolenga kusaidia jitihada za Serikali katika kuboresha elimu.” Alisema Bi. Ruth Zaipuna.
“Kwa kuanzia, leo tunamkabidhi Mkuu wa Mkoa rimu za karatasi 1,500 na taulo za kike, kwa ajili ya wanafunzi wa mkoa wake wanaojiandaa na kambi za mitihani. Habari njema ni kuwa, tamasha hili limeanzia Dodoma, ila litasambaa kote nchini na tamasha lijalo hapa litakuwa majira ya mvua na tutalitumia kupanda miti kuibadili Dodoma kuwa ya kijani,” alisisitiza Zaipuna.
Aidha, Zaipuna alimhakikishia Makamu wa Rais Dk. Mpango kuwa, NMB ni benki bora na imara, yenye mtaji mkubwa na weledi wa kutosha kuhakikisha wateja wao na Watanzania wanapata huduma rafiki.
Naye Dk. Mpango hakuficha hisia zake juu ya malengo chanya yanayoambatana na tamasha hilo, ambapo alisisitiza Tamasha hili kuwa muhimu sana na aliwapongeza NMB, sio tu kwa ajili ya kuwezesha mazoezi na kujenga afya, bali kutokana na malengo chanya yaliyomo ya kusaidia elimu na mazingira kupitia Programu ya upandaji miti na aliahidi kuwa bega kwa bega na NMB katika ajenda ya upandaji miti.