Na. Veronica Mwafisi-RUFIJI na KILOSA
06 Septemba, 2021
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya kimkakati ambapo ikikamilika itatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi.
Dkt. Ndumbaro aliyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi na watumishi wa ofisi yake wa kada mbalimbali ya kutembelea miradi ya kimkakati ukiwemo Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) uliopo Wilayani Rufiji na Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) uliopo Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.
Katika ziara hiyo, Dkt. Ndumbaro amewasihi Watumishi wa Umma kufanya kazi kwa juhudi na kuendelea kuiunga mkono serikali ya Awamu ya Sita ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa haraka na kuwa na matokeo chanya.
“Niwaombe Watumishi wa Umma muendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo hii ya kimkakati ili ikamilike kwa wakati, hivyo kila mmoja wetu afanye kazi kwa uadilifu, uzalendo na kwa juhudi ili iweze kuzaa matunda katika kuleta maendeleo ya nchi yetu,” Dkt. Ndumbaro ameongeza.
Dkt. Ndumbaro amesema ameamua kuambatana na watumishi wa kada mbalimbali wa ofisi yake ili kuwa na uwakilishi mzuri wa watumishi wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki katika kujionea juhudi zinazofanywa na Serikali katika miradi hiyo ya kimkakati kwa lengo la kuwa mabalozi wazuri wa shughuli zinazofanywa na serikali.
Naye Mkurugenzi Rasilimaliwatu na Utawala (TRC), Bi. Amina Lumuli ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia kwa mchango mkubwa wanaowapa katika kutekeleza ujenzi wa mradi huo ambao mpaka sasa kipande cha kwanza kimefikia asilimia 98.
Bi. Lumuli amemshukuru na kumpongeza Dkt. Laurean Ndumbaro kwa kuwapeleka watumishi wa ofisi yake katika mradi hiyo ili kujionea maendeleo ya ujenzi huo.
Bi. Lumuli amemuomba Dkt. Ndumbaro, kuwapatia ushirikiano pale watakapotaka kuajiri watumishi wenye taaluma mbalimbali pamoja na kuwapatia mafunzo watumishi hao watakaokuwa wanaendesha reli hiyo ya kisasa.
Mmoja wa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimemti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, walioshiriki ziara hiyo, Bw. Humfrey Mbuma, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwao kwani wamejionea jinsi miradi hiyo inavyotekelezwa kwa fedha za Watanzania ambapo mradi wa JNHPP utapunguza au kumaliza tatizo la umeme nchini.
“Tunaishukuru na kuipongeza Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia kwa kutekeleza mradi huu na mingine mingi ya kimkakati, Watanzania tumefurahi, tutaendelea kumuunga mkono kwa kuchapa kazi kama tunavyosema Kazi Iendelee,” amesema.
Kwa upande wao Watumishi Josephine Manase na Maynesy Mollel wamemshukuru Dkt. Ndumbaro kwa kuwapa fursa watumishi wa ofisi yake ya kutembelea miradi ya kimkakati na kuahidi kuwa mabalozi wazuri katika kuelezea umuhimu wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Cosmas Ngangaji amesema miradi hiyo ni mizuri sana kwa maslahi mapana ya nchi, hivyo hatuna budi kuwapongeza waliowaza kuianzisha, walioidhinisha na walioanza utekelezaji wake.
Katika ziara hiyo, kwa upande wa JNHPP watumishi hao wametembelea ujenzi wa tuta kuu la kuzuia maji, ujenzi wa handaki tatu za kupeleka maji kwenye mitambo zenye urefu wa mita 550 kila moja, ujenzi wa kituo cha kupokea na kusafirisha umeme ulioongezwa nguvu kutoka kilovoti 15.7 hadi kilovoti 400 chenye urefu wa mita 400 pamoja na ujenzi wa nyumba za makazi za kudumu za watumishi watakaokuwa wakiendesha mitambo pindi mradi huo utakapokamilika pia wamefanikiwa kutembelea Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na kujionea handaki lililopo chini ya mlima ambalo reli hiyo ya kisasa itapita.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.Laurean Ndumbaro akipewa maelezo na Mkandarasi Mshauri Mhandisi John Mageni kuhusu vifaa vilivyotumika kwenye reli hiyo iliyopita ndani ya handaki wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea mradi huo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro. Wengine ni watumishi wa ofisi yake aliombatana nao kwenye ziara hiyo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.Laurean Ndumbaro akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa ofisi yake wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea Ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) Wilayani Kilosa mkoani Morogoro. Kulia kwake ni Mkurugenzi Rasilimaliwatu na Utawala (TRC) Bi. Amina Lumuli na wengine ni wafanyakazi wa ujenzi wa mradi huo.
Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakitazama michoro ya Ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kabla ya kuingia kwenye handaki ambapo reli hiyo imepita wakati wa ziara ya kikazi waliyoifanya Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakielekea kutazama ujenzi wa jengo la mitambo (power house) ikiwa ni moja ya Mradi wa Kufua Umeme kwa nguvu za maji wa Julius Nyerere wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea mradi huo uliopo Wilayani Rufiji.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (wa kwanza kushoto toka kwa Mhandisi Mageni aliyeshika kipaza sauti) akimsikiliza Mkandarasi Mshauri Mhandisi John Mageni (aliyeshika kipaza sauti) alipokuwa akiwaonyesha ujenzi wa tuta kuu la kuzuia maji wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo na watumishi wa ofisi yake ya kutembelea Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere uliopo Wilayani Rufiji. Wa kwanza kulia toka kwa Mhandisi Mageni ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI Dkt. Francis Michael.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (Kushoto) akimsikiliza Mkandarasi Mshauri Mhandisi John Mageni alipokuwa katika ziara ya kikazi na watumishi wa ofisi yake ya kutembelea Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere uliopo Wilayani Rufiji. Nyuma yake ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael.