**************************************
Jamii imetakiwa kushiriki shughuli za michezo kwaajili ya kuimarisha afya ya mwili na kuifanya sekta hiyo kuwa ajira ili kujikwamua kiuchumi
Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela Bi Aziza Isimbula wakati akifungua mchezo wa robo fainali Kati ya timu ya kata ya Kirumba na timu ya kata ya Nyasaka katika viwanja vya shule ya msingi Sabasaba ikiwa ni muendelezo wa mashindano ya Angeline Jimbo Cup 2021 ambapo ameiasa jamii kushiriki katika michezo kwaajili ya kuimarisha afya pamoja na kujipatia kipato kwa kujiajiri katika michezo
‘.. Dhamira ya Mbunge ni kuibua vipaji, Lakini tushiriki michezo kwaajili ya afya zetu pia kama ajira, Na huu ni utekelezaji wa Ilani yetu ya uchaguzi ..’ Alisema
Aidha Katibu Aziza amempongeza na kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula Kwa kuendesha mashindano hayo hivyo kuwataka vijana kuitumia vizuri fursa hiyo katika kuondoa umasikini.
Kwa upande wake Kocha wa timu ya kata ya Kirumba Jonas Julius amesema kuwa kitendo Cha timu yake kupata ushindi wa kufuzu nusu fainali dhidi ya timu ya kata ya Nyasaka kimetokana na wachezaji wa timu hiyo kutokata tamaa mara baada ya kufungwa goli moja katika kipindi cha kwanza sambamba na kuahidi ushindi wa mashindano hayo katika hatua inayofuata huku akiomba mashabiki kuzidi kuiunga mkono timu hiyo
Nae Kocha wa timu ya kata ya Nyasaka Jumanne Samson amefafanua kuwa wachezaji wake hawapaswi kulalamika Kwa matokeo walioyapata kwani walipata fursa nyingi za ushindi wakashindwa kuzitumia badala yake amewataka kujipanga upya kwaajili ya msimu ujao huku akimpongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela Kwa kubuni mashindano hayo
Timu ya kata ya Kirumba imefanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali dhidi ya Nyasaka baada ya kushinda kwa mikwaju ya penati 4 Kwa 3 kabla ya matokeo sare ya goli moja Kwa moja katika mchezo wa dakika tisini.