Afisa Uhusiano na Huduma kwa wateja Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Chanika Bi. Mwanaisha Mbita (upande wa kushoto) akiwa na Afisa Uhusiano na Huduma kwa wateja TANESCO Mkoa wa Ilala Bw. Deusdedit Hokororo wakiwa katika kikao na wananchi wa Kata ya Msongola kwa ajili ya kusikiliza kero zao, kuwapa elimu na kuwajengea uelewa namna wanavyotekeleza majukumu yao pamoja na kutatua changamoto.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa wateja Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Chanika Bi. Mwanaisha Mbita akitoa elimu kwa wananchi wa Kata ya Msongola kuhusu utaratibu wa kupata huduma ya umeme.
Diwani wa Kata ya Msongola Bw. Azizi Mwalile akizungumza jambo katika kikao kati wananchi wa Msongola na TANESCO Mkoa wa Ilala kwa ajili ya kusikiliza kero zao, kuwapa elimu na kuwajengea uelewa namna wanavyotekeleza majukumu yao pamoja na kutatua changamoto.
Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa Mbondole Kata ya Msongola Bw. Thomas Nyanduli akizungumza jambo katika kikao kati ya wananchi wa Msongola na TANESCO ambacho kimelenga kusikiliza kero pamoja na kutatua changamoto mbalimbali katika kupata huduma ya umeme.
Mkazi wa Kata ya Msongola Bi. Kasiana Mhagama akiwasilisha kero kwa watendaji wa TANESCO Mkoa wa Ilala katika kikao kilichowakutanisha wananchi kwa ajili ya kupewa elimu na kutatua changamoto katika kupatiwa huduma za umeme.
Wananchi wa Kata ya Msongola wakiwa katika kikao na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ilala kwa ajili ya kusikiliza kero zao, kuwapa elimu na kuwajengea uelewa namna wanavyotekeleza majumu yao pamoja na kutatua changamoto.
……………………………………………………………………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ilala wapo katika mpango wa kupeleka nguzo za umeme katika Wilaya ya Chanika kwa ajili ya kutatua changamoto ya ukosefu wa miundombinu ya umeme kwa baadhi ya maeneo.
Hatua hiyo imekuja baada ya TANESCO Mkoa wa Ilala kufanya kikao na wananchi wa Kata ya Msongola kwa ajili ya kusikiliza kero, kuwapa elimu na kuwajengea uelewa namna wanavyotekeleza majumu yao pamoja na kutatua changamoto.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na wananchi wa Kata ya Msongola Afisa Uhusiano na Huduma kwa wateja Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ilala Bw. Deusdedit Hokororo, amesema kwa sasa wapo katika mchakato wa kutafuta nguzo za umeme kwa ajili ya kupeleka katika maeneo ambayo hakuna umeme.
Bw. Hokororo amesema kuwa nguzo hizo za umeme zitatumika katika maeneo yote ambayo wananchi wamekosa huduma ya umeme muda mrefu.
“Tumeomba kwa viongozi wetu wa juu kupatiwa nguzo za umeme kwa ajili ya TANESCO Wilaya ya Chanika ili kila mteja wetu apate huduma kwa wakati” amesema Bw. Hokororo.
Amefafanua kuwa kila mtu anatakiwa kujiandaa kwa ajili ya kupata huduma ya umeme kutokana hivi karibuni wanatarajia kuanza kuleta miundombinu.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa wateja TANESCO Wilaya ya Chanika Bi. Mwanaisha Mbita, amesema kuwa hatua ya kwanza ili mteja apate umeme anatakiwa kufika katika ofisi za TANESCO kwa ajili ya kuchukua fomu akiwa na nakala ya kitambulisho pamoja na picha.
Bi. Mbati amesema baada ya mteja kuchukua fomu na kurudisha anatakiwa hakikisha nyumba yake imefanyiwa mfumo wa umeme vizuri (wiring) pamoja kuwa na mchoro sahihi kutoka kwa mtaalam wa umeme.
“Ukirudisha fomu mteja unapangiwa tarehe ya survey kuja katika nyumba yako kukagua wiring ya umeme, hakuna gharama ya yoyote na baada ya hapo unapewa namba ya malipo na kwenda kulipia Sh. 27,000 ” amesema Bi. Mbati.
Amefafanua kuna aina nyingi za kufanya malipo ikiwemo njia ya benki au mtandao wa simu ambapo mitandayo yote inakupokea malipo ya serikali.
“Baada ya kufanya malipo taarifa itatufikia kuwa mteja fulani tayari amefanya malipo, naomba tufate taratibu za kiofisi ili kuepuka matapeli “amesema Bi. Mbati.
Wananchi wa Kata ya Msongola wamepata fursa ya kuwasilisha maoni yao, ambapo wameiomba TANESCO kuhakikisha wanafikisha huduma ya umeme katika maeneo yote.