Meneja wa Kampuni ya eMo Bodaboda Bw. George Laurian (kulia) akitoa elimu kwa Mkazi wa Manispaa ya Kigamboni kuhusu pikipiki inayotumia mfumo wa umeme.
Mwanzilishi na Mkurugenzi wa eMo Bodaboda Bw. Erick Morro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu pikipiki zinazotumia mfumo wa umeme.
*********************.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Mtanzania anayemiliki Kampuni ya eMo Bodaboda ameanza kutekeleza agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufikia uchumi wa viwanda baada ya kubuni teknolojia ya mpya ya pikipiki inayotumia mfumo wa umeme.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mwanzilishi na Mkurugenzi wa eMo Bodaboda Bw. Erick Morro, amesema kuwa lengo la teknolojia ya pikipiki inayotumia mfumo wa umeme ni kusaidia jamii wakiwemo hasa vijana katika kujikwamua kiuchumi.
Bw. Morro amesema kuwa mfumo wa pikipiki ya umeme ni rafiki kwa kila mtu kutokana pikipiki hizo hazitumii mafuta, oili na zinauwezo kwenda mwendo wa kilometa 80 na kubeba mzigo kilo 100.
”Teknolojia hii nimeitoa nchini Ujerumani na zinauwezo wa kutumia saa 8 bila betri kuisha chaji, azitoe mlio hivyo ni rafiki kwa kila mtu” amesema Bw. Morro.
Ameeleza kuwa wanaendelea kuelimisha jamii kuhusu teknolojia hiyo mpya ambapo mwitikio wake ni mkubwa kwani wadau wanajitokeza kupata elimu ya mfumo huo wa umeme.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii namna ya kutumia pikipiki za eMo, kwani tupo katika hatua ya awali ya kufanya utafiti kwa ajili ya kufanya uwekezaji” amesema Bw. Morro.
Amefafanua wapo katika mazungumzo ya awali na Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) kwa ajili ya kuwajengea vijana uwezo ambao utawasaidia kujua teknolojia ya eMo bodaboda na kuongeza fursa za ajira.
Bw. Morro amewataka wadau mbalimbali kuja kuwekeza ili waweze kuingia nao ubia kwa ajili ya kufungua kiwanda ambacho kitakuwa kinazalisha pikipiki zenye mfumo wa umeme.
“Lengo langu baada ya mwaka mmoja tutakuwa na teknolojia ya kuzibadilisha hizi pikipiki za kawaida kuwa na mfumo wa umeme” amesema Bw. Morro.