Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akizungumza na Maafisa Magereza katika Gereza la Mahabusu Segerea jijini Dar Es Salaam, alipofanya ziara kwenye gereza hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jami Dkt. John Jingu akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Magereza wa Gereza la Mahabusu Segerea jijini Dar Es Salaam, mara baada ya ziara kwenye gereza hilo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akisoma baadhi ya vielelezo alivyokabidhiwa katika Gereza la Mahabusu Segerea mara baada ya ziara yake Gerezani hapo kushoto kwake ni Mkuu wa Gereza Msaidizi, Gereza la Mahabusu Segerea, Mrakibu wa Magereza, Athanas Ndowano.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akitoka katika Gereza la Mahabusu, Segerea Jijini Dar es Salaam mara baada ya ziara yake Gerezani hapo, kushoto kwake ni Mkuu wa Gereza Msaidizi, Gereza la Mahabusu Segerea , Mrakibu wa Magereza, Athanas Ndowano na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Lucy Saleko.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WAMJW
**********************************
Na Mwandishi Maalum
Serikali imewahakikishia wafungwa na mahabusu nchini kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili hususani zinazohusu masuala ya Ustawi wa Jamii wakiwa magerezani kwa kuzingatia taratibu zote kama ilivyo kwa makundi mengine.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar Es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu katika ziara yake ya kikazi kwenye Gereza la Mahabusu ya Segerea.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Dkt. Jingu amesema kuwa ziara hiyo imekuwa ya mafanikio kwake na wataalam alioongozana nao na imewafumbua macho juu ya utendaji kazi ndani ya gereza, changamoto zinazowakabili mahabusu na wafungwa na namna ya kuzitatua.
Katika ziara hiyo Dkt. John Jingu amekiri kujifunza mambo mengi yatakayoiwezesha Wizara kuboresha utendaji kazi wake hususan makundi inayoyasimamia yakiwemo wanawake na watoto na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wakiwa mahabusu na wafungwa zinatatuliwa.
“Tumekuwa na ziara za aina hii katika magereza mbalimbali nchini na tutahakikisha tunafika katika magereza yote na tunatafuta namna bora zaidi ya Ustawi wa Jamii wa makundi ya wafungwa na mahabusu katika magereza wakwiemo Wanawake na Watoto waliokinzana na Sheria” alisema Dkt. Jingu.
Ameongeza kuwa makundi hayo ni sehemu ya jukumu kubwa la Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ambayo inasimamia masuala ya Jinsia, Wazee na Watoto na maendeleo kwa ujumla wake hivyo, ziara za aina hiyo zinaongeza uelewa kuhusu masuala yanayoendelea katika maeneo kama haya ya magereza.
“Tumejifunza mambo mengi kutoka kwa wahusika hawa, na uelewa huu utatuwezesha kuboresha utendaji kazi wetu kama Wizara na pale kwenye matatizo ya kijamii tunajengewa uwezo kuhusu namna kupata ufumbuzi wa matatizo ya kijamii kwa matendo badala ya kuongozwa na nadharia” alisisitiza.
Aidha, ameitaka jamii kujitafakari kuhusu matendo yanayosababisha wanajamii kujikuta wanakinzana na Sheria na wakati mwingine kutafuta mbinu za kuepusha migogoro ya kijamii ili kujiepusha kuangukia gerezani.
Akiwa katika Gereza hilo, Katibu Mkuu Jingu alipata fursa ya kuzungumza na mahabusu waliochini ya miaka 18 (watoto), pamoja na mahabusu na wafungwa wanawake.
Akizungumzia ziara ya Katibu Mkuu katika Gereza la Segerea, Mkuu wa Gereza Msaidizi Gereza hilo, Mrakibu wa Magereza, Athanas Ndowano amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa Ustawi na Maendeleo ya Jamii na inaweza kuboresha na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
“Nasema ziara za aina hii ni nzuri na zitatusaidia kuboresha huduma katika magereza yetu kwa sababu Wizara inayosimamia maendeleo na Ustawi wa Jamii inasikiliza changamoto zetu pamoja na changamoto za wafungwa na mahabusu hivyo tutapata ufumbuzi wa changamoto hizo na naamini zitapungua kwa kiasi kikubwa,” alisema Ndowano.