Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali ya wabunge, bungeni jijini Dodoma, September 2, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeshatoa sh. bilioni 15 kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kununua mahindi kutoka kwa wakulima.
“Uzalishaji wa mahindi ni mkubwa lakini na sisi pia tumeimarisha hifadhi yetu ya Taifa ya chakula. NFRA tumeipa fedha za kwenda kununua mahindi kwa bei ya kumwezesha mkulima ili ajikimu hadi msimu ujao. Uwezo si mkubwa sana, lakini tumeipa shilingi bilioni 15,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 2, 2021) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kwela, Mheshimiwa Deus Clement Sangu kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesema siku nne zilizopita alikuwa ziarani mkoani Katavi na aliona hali halisi ya mlundikano wa mahindi na akakutana na watu wa NFRA ili aone kasi yao ya ununuzi ikoje.
“Nilibaini kuwa uwezo wao ni mdogo na nikapokea malalamiko ya wananchi kwamba kituo cha kupokelea mahindi kiko mbali, kwa hiyo tumeamua kuanzia sasa kila Halmashauri itapaswa iwe na kituo japo kimoja cha kupokelea mahindi ili kuharakisha ununuzi wa zao hilo.”
“Tunawahakikishia wakulima wetu kwamba tunanunua mahindi kupitia NFRA na Bodi ya Mazao Mchanganyiko na pia tumefungua milango kwa yeyote anayetaka kuuza mahindi nje. Mtu akitaka kuuza mahindi Zambia, Congo, Msumbiji au Malawi yuko huru kufanya hivyo ili mradi atoe taarifa ili nasi tujue tumeuza kiasi gani,” amesema wakati akimjibu Mhe. Sangu ambaye alitaka kujua Serikali imejipanga vipi kuziwezesha taasisi za Serikali kama NFRA ili ziweze kununua mahindi ya wakulima.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuunganisha taasisi za NIDA na RITA kutokana na tofauti za majukumu yake. Alikuwa akijibu swali la Mhe. Abubakari Damian Asenga, mbunge wa Kilombero ambaye alishauri taasisi hizo ziunganishwe ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa ambavyo alisema kwa sasa vinacheleweshwa sana.
“NIDA inatoa kitambulisho cha Taifa ambacho kinamtambulisha Mtanzania na hakitolewi kwa mtu ambaye si raia wakati RITA inatoa cheti cha kuzaliwa kikionesha kuwa umezaliwa wapi, tarehe yako ya kuzaliwa na pia wanatoa cheti cha kifo.”
Amesema RITA inaweza kutoa cheti cha kuzaliwa kwa mtu yeyote aliyezaliwa Tanzania kwa sababu pale hospitalini akishazaliwa mtoto, taarifa zitaonesha hivyo na inaweza kutoa cheti kwa huyo mtoto huyo hata kama siyo Mtanzania.
“Mtu anaweza kuzaliwa Tanzania na kupewa cheti cha kuzaliwa kwa kuwa amezaliwa ndani ya nchi yetu, lakini mtu huyo anaweza asiwe Mtanzania kwa mujibu wa sheria zetu.”
Amesema taasisi hizo zinaweza kupeana taarifa pale inapobidi lakini vyote vina majukumu tofauti. “Urasimu unaosemwa hapa nimeusikia wakati nilipofanya ziara kwenye mikoa ya pembezoni. Na huko nimekuwa nikisisitiza umakini katika kuchunguza taarifa za waombaji.”
“Kuchelewa kwetu kwenye mikoa ya pembezoni ambako pia kunaitwa urasimu, kunafanywa kwa nia nzuri ili kujiridhisha kama kweli anayeomba kitambulisho ni raia wa Tanzania,” amesisitiza.
“Nataka niwahakikishie Watanzania kwamba mtu yeyote Mtanzania ambaye Baba na Mama ni Watanzania, ni lazima atapata kitambulisho cha Taifa, kikubwa wawe na subira. Nasi kwa upande wetu tumejitahidi kuongeza vifaa na watumishi ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo hasa kwa wale ambao wamehakikiwa na wanastahili.”