Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF akizungumza leo Kuhusu usajili wa vituo elfu 800 vinavyohudumia wanachama wa mfuko huo.
Meneja Uhusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF Bi. Angella Mziray akifafanua jambo katika mkutano huo.
*******************************
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mpaka sasa umesajili Vituo vya kutolea huduma zaidi ya 8,000 vinavyohudumia wanachama wa Mfuko huo ambavyo vinajumuisha maduka ya dawa, vituo vinavyomilikiwa na Serikali, mashirika ya dini na watu binafsi kuanzia ngazi ya Zahanati hadi ngazi ya Taifa.
Uwepo wa vituo hivi ni ishara nzuri ya upatikanaji wa huduma kwa wanachama kiurahisi, lakini pamoja na uwepo wa vituo hivi bado zipo changamoto za hapa na pale hivyo kupitia kikao hiki changamoto hizi zitajadiliwa na kufikia maamuzi ya pamoja ya namna ya kukabiliana nazo.
Ameyasema hayo leo Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe.Hassan Rwaga akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano wa watoa huduma za afya na NHIF Jijini Dar es salaam tarehe 2 Septemba 2021.
Amesema Serikali imeshawekeza kwa kujenga vituo vyenye mazingira mazuri mpaka ngazi za chini na inaendelea kuongeza bajeti ya afya kuhakikisha miundombinu na rasilimali watu zinatosheleza katika kutoa huduma bora.
“Hakuna sababu ya kuwa na huduma mbaya kwa sasa kutokana na nguvu kubwa ya Serikali iliyoelekezwa katika uimarishaji na upatikanaji wa dawa na vitendanishi katika vituo vyote vya Serikali”. Amesema
Aidha ameipongeza NHIF na Watoa huduma ambao wameweza kuunganisha mifumo yao na kurahisisha kwa kiasi kikubwa ushughulikiaji wa malipo ya madai.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga amesema Mfuko umekuwa ukifanya kazi zake kwa kuongozwa na dhana ya ushirikishwaji na uwazi kwa wadau wake wote mkiwemo Watoa Huduma wanaohudumia wanachama wa Mfuko huu.
Amesema Mfuko umekuwa ukiutumia katika kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza lakini bado tumeendelea kushuhudia kuwepo kwa malalamiko hasa yanayohusu kucheleweshewa malipo ya madai yenu,malalamiko ambayo yamekuwa yakipitia njia zisizo rasmi hivyo niwaombe sana kuutumia muda huu kuwa wawazi kusema changamoto mlizonazo ili wote kwa pamoja tuzijadili kwa kina na kupata suluhu.
Pamoja na hayo amesema Malipo kwa Watoa huduma kwa sasa yanalipwa ndani ya muda mfupi zaidi wa kati ya siku 30 hadi 45 ikilinganishwa na awali ambapo ilikuwa ni siku 60 na wakati mwingine kuzidi na kufikia 100. Aidha malipo hayo yamewezesha vituo kuwa na mapato ya uhakika ambayo yanawezesha vituo kuimarisha huduma.