Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
KAMISAA wa Sensa Tanzania Bara Anne Makinda amekemea baadhi ya wananchi kuingiza masuala ya kisiasa kwenye sensa inayotarajia kufanyika mwaka 2022 .
Pamoja na ile ya majaribio itakayofanyika mwezi huu.
Makinda aliyasema hayo alipokuwa akiongea na wakazi wa Mtaa wa Muheza Wilaya ya Kibaha eneo ambalo ni kati ya vituo 13 vitakavyoshiriki sensa ya majaribio inayofanyika usiku wa Septemba 10 kuamkia 11.
Alieleza,kupitia sensa ambayo inatarajiwa kufanyika 2022 Serikali inaweza kupanga mipango ya maendeleo bila shida hivyo .
“Pia ni marufuku kwa karani kutangaza habari za mtu, mwananchi usiwe na sababu ya kutojiandikisha semeni ukweli mtakapokuwa mnatoa taarifa zenu ziko sehemu salama” alisema.
Makinda alisema uzinduzi wa sensa utafanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu mwezi huu mara baada ya kufanyika kwa sensa ya majaribio katika vituo 13 ambavyo tayari vimeainishwa.
Alisema sensa ya 2022 itakuwa ya tofauti na zilizotangulia kwani itaanzia ngazi ya vitongoji tofauti na ilivyokuwa awali ambayo ilikuwa inafantyika kwenye wilaya.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kufanyika kwa sensa ni jambo la muhimu kwa mkoa huo ambao una migogoro ya ardhi, kujua namna ya kupanga mifugo na watu kwenye maeneo husika.
Kunenge alisema sensa itasaidia pia mkoa huo kupanga masuala ya kiuchumi, mipango miji na viwanda ambapo alieleza kuwa kwasasa ipo sensa ya mifugo inaendelea kufanywa katika mkoa wa Pwani.
“Sasa hivi mkoa una migogoro ya wakulima na wafugaji bila kujua idadi ya watu na mkfugo ni ngumu kupanga idadi gani ya mifugo inahitajika kwenye eneo husika” alisema Kunenge.
Afisa wa Sensa Said Ameir alisema karani wa sensa ambaye atabainika kutotunza siri za watu ipo adhabu ambayo inachukuliwa hivyo wananchi wanatakiwa kuwa huru kutoa taarifa sahihi.