Watoa huduma za afya katika ngazi za kata na vijiji wametakiwa kutembelea nyumba kwa nyumba ili kuwatambua mama wajawazito na watoto walioko maeneo hayo ili kuwapatia ushauri wa kiafya kwa kuwa hao ndio wateja wao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Satano Mahenge ametoa kauli hiyo leo tarehe 31.08.2021 alipokuwa akifungua kikao kazi cha Wataalam wa afya wa Mkoa wa Singida kilichokuwa kinajadili tathmini na vifo vya kinamama vitokanavyo na uzazi pamoja na vifo vya watoto wachanga kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Akifungua kikako hicho Dkt. Mahenge amesema kwamba bado kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza au kuondoa vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi pamoja na watoto wachanga endapo wataalamu wa afya ngazi ya kata na vijiji watatembelea nyumba kwa nyumba kuangalia uwepo wa watu hao na kuwapatia ushauri wa kwenda hospitali kwa wakati na kutumia lishe bora kwa afya ya mama na mtoto.
“Kutembelea nyumba kwa nyumba kutasaidia kujua idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya afya na ushauri katika eno husika, hii inatokana na ukweli kwamba wanawake wengi huchelewa kuanza kiliniki pindi wanapokuwa wajawazito na kusababisha matatizo wakati wa kujifungua” alikaririwa Dkt. Mahenge.
Amesema Serikali ya awamu ya sita chini Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kujenga miundombinu wezeshi kwa sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti na idadi ya watumishi katika sekta hiyo ili kusogeza huduma na elimu ya afya kwa wanachi.
Amesema ujenzi na uboreshwaji wa vituo vya afya ni mkakati wa Serikali wa kuondoa changamoto ya vifo vya kinamama vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga.
Hata hivyo Dkt. Mahenge amebainisha kwamba jumla ya vituo vya afya 15 na hospitali tatu (3) zimejengwa mkoani hapo ili kusaidia utoaji wa huduma za dharura kwa wazazi na watoto.
Aidha Mhe. Mahenge amezitaka Halmashauri mkoani hapo kuhakikisha kwamba vituo vyote vya kutolea huduma ya afya vinakuwa na mikakati ya kupunguza au kuondoa vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi pamoja na changamoto ya vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika.
Pia amezitaka Halmashauri kuimarisha upatikanaji wa bidhaa afya kutoka MSD na kwa mshitiri hasa kwa bidhaa za mama na mtoto kama vile vifaa tiba vya kupimia wingi wa damu, kuhakikisha uwepo wa dawa za kuongeza damu katika vituo vyote pamoja na dawa muhimu za kuzuia damu kutoka baada ya kujifungua na matibabu mengine muhimu katika kundi hili.
Awali Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Victorina Ludovick amesema lengo la kikao kazi hicho ni kujadili na kutathmini vifo vya kinamama vilivyosababishwa na uzazi vilivyotokea kwa muda wa miezi mitatu ya April hadi Juni 2021 ambapo kikao hicho kitatoa suluhisho la namna ya kuzuia hali hiyo isiweze kujirudia.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kinategemewa kutoa mrejesho wa matukio kadhaa ya vifo vilivyojitokeza na kujadili mipango kazi ya Halmashuari hizi kwa kipindi cha miezi mitatu na kuchukua hatua stahiki za kuboresha maeneo yenye changamoto, alisema Dkt.Victorina
Aidha alibainisha kwamba bado kuna changamoto ya jamii yetu kwenye kupanga uzazi na pia vijana kupata mimba wakiwa katika umri mdogo ambapo wengi wao hupoteza maisha kwa kutokwa na damu vyingi wakati wa kujifungua.
“Bado tuna changamoto ya ukusanyaji wa damu salama ambayo hutumika kuwasaidia kinamama na watoto wanapokuwa na uhitaji”. Alisema Mganga Mkuu wa Mkoa
Dkt. Victorina amewaomba wananchi wa mkoa huo kuendelea kuchangia damu ili iweze kuwasaidia wenye uhitaji.
Hata hivyo Mganga Mkuu amewataka wahudumu wa afya kuendelea kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa wananchi kwa kuwa itawezesha kuwa na uzazi salama na pia ina mchango mkubwa katika kuzuia vifo vya kinamama vinavyosababishwa na uzazi.
Naye Emanueli Mlalange Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Itigi na Mwenyekiti wa Waganga wakuu wa mkoa huo kwa niaba ya waganga hao ameishukuru serikali kwa jitihada zake za kuongeza watumishi mkoani hapo na kuimarisha utoaji wa dawa katika vituo vya afya.
Aidha amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba madaktari watajitahidi kuhakikisha kwamba vifo vya kinamama na watoto wachangavinapungua.
Mwisho