KATIKA kuunga mkono azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inakua Nchi ya Kidigitali, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Chamwino Mkoani Dodoma, Deo Ndejembi amegawa Kompyuta Tano kwenye Shule ya Sekondari Buigiri.
Ndejembi amesema mbali na kugawa Kompyuta hizo pia amegawa printa moja kwa ajili ya kusaidia uchapaji wa mitihani na hivyo kuokoa gharama za Shule kwenda kuchapa mitihani sehemu nyingine.
Amesema ugawaji wa vifaa hivyo vya kidijitali hautoishia katika Kata ya Buigiri pekee yake bali atahakikisha anazifikia Shule zote zilizopo katika Jimbo lake Ili kuweza kurahisha shughuli za ufundishaji na kujifunzia kwa Walimu na Wanafunzi.
” Leo nimefanya ziara katika Kata ya Buigiri ambapo nimetembelea Shule ya Sekondari Buigiri ambapo nimewakabidhi Kompyuta Tano na Printa moja ambazo naamini zitawasaidia Walimu kufanya kazi zao kwa ufanisi ikiwemo kuchapishia Mitihani na kuhifadhi nyaraka mbalimbali za Shule yao.
Hizi zote ni katika kuunga mkono jitihada za Rais wetu Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha tunakua na Tanzania ya Kidijitali, tumeanza Kata ya Buigiri kesho ntafika katika Sekondari ya Kata ya Majereko na Kata ya Haneti,” Amesema Naibu Waziri Ndejembi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi amemshukuru Naibu Waziri Ndejembi ambapo amesema upatikanaji wa vifaa hivyo utawasaidia Walimu kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Nae mmoja wa wanafunzi wa Shule hiyo, John Pius amemshukuru Mbunge wao kwa kutimiza ahadi ambayo aliitoa alipofika kwenye shule hiyo Januari mwaka huu ambapo amesema vifaa hivyo vitawasaidia wao na walimu wao katika kujifunza kidijitali.