Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia), akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya NMB Kama Upepo inayolenga kuchagiza matumizi ya kadi za NMB mastercard na QR kwa ajili ya kununua tiketi za ndege za Skylink. Kutoka kushoto ni Meneja Uendeshaji wa Skylink, Solomon Mwale, Mkurugenzi wa Skylink, Moustafa Khataw na Mkuu wa Idara ya Biashara za Kadi NMB, Philbert Casmir.
Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Skylink, Moustafa Khataw wakizindua kampeni ya NMB Kama Upepo inayolenga kuchagiza matumizi ya kadi za NMB mastercard na QR code kwa ajili ya kununua tiketi za ndege za Skylink.Kushoto ni Meneja Uendeshaji wa Skylink, Solomon Mwale na kulia ni Mkuu wa Idara ya Biashara za Kadi NMB, Philbert Casmir.
………………………………………………………………………………..
Benki ya NMB imezindua kampeni ya ‘NMB Kama Upepo,’ iliyotokana na Makubaliano ya Kibiashara na Kampuni ya Skylink Travel & Tours, inayojihusisha na uwakala wa tiketi za ndege – kuwazawadia washindi sita na wenza wao safari iliyolipiwa gharama zote kwa siku tatu nchini Dubai.
‘NMB Kama Upepo’ ni kampeni itakayoendeshwa kwa miezi mitano, ikilenga kukuza matumizi ya kadi za NMB mastercard na QR Code miongoni mwa wateja wa benki hiyo kwa ajili ya kununua tiketi za ndege, ambako watapata punguzo la asilimia 60 ya ada ya huduma (service charges).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ‘NMB Kama Upepo’, uliofanyika jijini Dar es Salaam , Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, alisema kampeni hiyo itakuwa na zawadi za kila wiki na kila mwezi kwa wateja wa NMB watakaofanya malipo ya tiketi za ndege kutoka Skylink kwa kutumia kadi za mastercard na QR Code.
“Kadri mteja atakavyotumia kadi katika manunuzi ya mitandaoni au kufanya malipo kupitia kadi za NMB kwenye tovuti ya Skylink, ama mashine zetu za malipo (POS) zilizoko katika ofisi za washirika wetu hawa, ndivyo atavyojiongezea nafasi za kushinda zawadi kutoka kwetu.
“Katika kipindi chote cha kampeni hii ya NMB Kama Upepo, inayoanza Septemba 1, 2021 hadi Januari 2022, washindi sita na wenza wao (jumla watu 12), tutawazawadia safari iliyolipiwa gharama zote, ikiwamo malazi kwa siku tatu huko Dubai, tiketi za ndege za kwenda huko na kurudi nchini, pamoja na pesa za matumizi,” alisema Mponzi.
Aidha, Mponzi alifafanua kuwa, NMB Kama Upepo ni kampeni chanya yenye lengo la kupunguza matumizi ya pesa taslimu na kwamba iko wazi kwa wateja wote wanaomiliki kadi za NMB mastercard, sambamba na wale wote ambao wameomba ama watakaoomba kadi mpya wakati kampeni hiyo ikiendelea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Skylink, Moustafa Khataw, alisema Skylink ina furaha kubwa sio tu kuingia makubaliano ya kibiashara na NMB, bali pia kuwa sehemu ya Kampeni ya NMB Kama Upepo, na kwamba wateja wa benki hiyo watafurahia huduma chanya zinazoenda kutolewa katika miezi yote ya uwepo wake.