Afisa biashara wa wilaya ya Igunga Mkoani Tabora Anthony Marco kulia wakipakia vitunguu kwenye gunia wakiwa na mchungaji Daniel Phares wa kanisa la FPCT Arusha mjini aliyemtembelea shambani kwake katika kijiji cha Itale kata ya Kitangili tarafa ya Simbo wilaya ya Igunga
Afisa biashara wilaya ya Igunga Anthony Marco akipulizia dawa katika shamba lake la vitunguu lililoko kijiji cha Itale kata ya Kitangili tarafa ya Simbo wilayani Igunga mkoani Tabora.
Shehena ya magunia 110 ya vitunguu vya afisa biashara Anthony Marco wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora akiwa amepakia kwenye lori baada ya kuvuna katika mashamba yake yaliyoko kijiji cha Itale kata ya Kitangili tarafa ya Simbo tayari kwa kusafirishwa kupelekwa kwenye soko la Kampala nchini Uganda kwa ajili ya kuuza .
………………………………………..
Na Lucas Raphael,Igunga
Wakati serikali ikitaka watanzania wawekeze kwenye kilimo cha mazao ya biashara hatimae afisa biashara wilaya ya Igunga mkoani Tabora Anthony Marco ameamua kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji cha zao la vitunguu ikiwa ni njia mojawapo ya kujiongezea kipato katika maisha yake ya kila siku.
Alitoa ushauri huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akipakia vitunguu vyake kwenye magunia baada ya kuvuna katika shamba lake lenye hekali 15 lililoko kijiji cha Itale kata ya Kitangili tarafa ya Simbo.
Anthony alisema siku za nyuma alikuwa akilima mazao ya choroko, mahindi, ufuta na pamba lakini hakuweza kupata mafanikio yoyote na alipoamua kubadilisha kilimo hicho na kulima kilimo cha zao la vitunguu amepata mafanikio makubwa.
Alisema kutokana na serikali kuhimiza kilimo cha umwagiliaji yeye aliamua kutafuta mashamba ya kukodi ambapo alipata maeneo mengi kwenye kata tatu za Kitangili Isakamaliwa na Igunga ambapo alifanikiwa kulima na kuvuna gunia 1500 kwa kilimo cha mihula miwili kila mwaka.
Alisema hivi sasa ameinuka kiuchumi kwani kutokana na kulima mfululizo tangu mwaka 2017 hadi 2021 amefanikiwa kununua gari ndogo ya kutembelea amejenga nyumba ya kisasa ya kuishi amenunua mashamba pia amenunua trekta yenye thamani ya Mil. 54 kwa ajili ya kupanua kilimo.
Aidha afisa biashara huyo aliongeza kuwa ameweza kununua pia mashine tatu za kumwagilia katika mashamba yake hata hivyo alibainisha kuwa kutokana na juhudi zake za kilimo kikubwa cha umwagiliaji benki ya NMB tawi la Igunga imempatia mkopo wa Mil. 80 ambapo ameishukuru benki hiyo huku akiahidi fedha hizo zote kuzitumia kwenye kilimo cha vitunguu.
Sambamba na hayo afisa biashara huyo alisema kutokana na yeye kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji ameweza kufanikiwa kuwapatia ajira vijana 88 kila mwaka ambapo wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali katika mashamba ikiwemo kupanga vitalu, kulima, kupanda vitunguu, kupiga dawa na kumwagilia.
Hata hivyo alisema kati ya hao 88 wanane amewapatia ajira za kudumu ambapo wawili anawalipa kwa mwezi kila mmoja 200,000/= na wengine sita anawalipa kwa mwezi kila mmoja 500,000/=.
Kufuatia hali hiyo amewashauri vijana wilayani Igunga kutumia nguvu zao kuwekeza kwenye kilimo cha vitunguu kwani zao hilo ni mkombozi mkubwa kwa kuinua maisha huku akisema kilimo ni moja ya ajira binafsi kwa kuwa fedha nyingi zipo kwenye kilimo endapo kila kijana atafanya kazi kwa kujituma pasipo kusubiri ajira toka serikalini.
Pamoja na kutoa wito kwa vijana alisema wilaya ya Igunga ina mito mingi na maji ya kutosha ambapo vijana wakitumia fursa hiyo umaskini kwao itabaki historia.
Sanjari na hayo alitoa wito kwa watumishi wa umma kutumia siku za jumamosi na jumapili kufanya shughuli binafsi za kujiingizia kipato ikiwemo kilimo cha vitunguu badala ya kutegemea mshahara.
Nao baadhi ya vijana waliopewa ajira na afisa biashara huyo katika mashamba yake Agnes Malale, Kisai Steven, Amina Jumanne kwa nyakati tofauti walisema kutokana na kazi wanazofanya katika mashamba hayo wamekuwa wakipata zaidi ya sh. 10,000 kwa siku ambapo fedha hizo zimewasaidia kujikwamua kimaisha huku wakumshukuru Anthony kwa kuwapatia ajira hiyo na kuwalipa kwa wakati.
Hata hivyo Amina alisema pamoja na kulipwa kiasi cha fedha hicho pia wamekuwa wakinufaika kwa kupata vitunguu vya kutumia kwenye mboga kwani hupewa bure na mwajiri wao ambapo amewataka baadhi ya vijana ambao wamekuwa na tabia ya kuilaumu serikali kuacha mara moja kwa kuwa ajira nyingi ziko kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Kwa upande wake meneja anayesimamia kusafirisha zao hilo la vitunguu katika soko la Kampala nchini Uganda Clement Masanja alisema wameamua kuuzia vitunguu Uganda kwa kuwa bei ya huko ni nzuri pia hakuna usumbufu wa malipo ya fedha.
Alisema bei ya gunia la vitunguu kwa Uganda ni sh. 240,000 ambapo kwa fedha ya Tanzania ni sh. 155,000/= huku akisema Tanzania gunia ni sh. 80,000 hadi 85,000 hata hivyo lazima ukopeshe vitunguu lakini Uganda unalipwa fedha taslimu.