Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 18 wa Wahandisi Prof.Bakari Mwinyiwiwa,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya maadhimisho hayo yanayotarajia kufanyika Septemba 2 hadi 3,2021 jijini Dodoma.Kulia ni Msajili wa Bodi ya Wahandisi (ERB) Mhandisi Patrick Barozi
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 18 wa Wahandisi Prof.Bakari Mwinyiwiwa,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya maadhimisho hayo yanayotarajia kufanyika Septemba 2 hadi 3,2021 jijini Dodoma.Kulia ni Msajili wa Bodi ya Wahandisi (ERB) Mhandisi Patrick Barozi
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 18 wa Wahandisi Prof.Bakari Mwinyiwiwa,wakati akitoa taarifa ya maadhimisho ya Mkutano huo unaotarajia kufanyika Septemba 2 hadi 3,2021 jijini Dodoma.
Msajili wa Bodi ya Wahandisi (ERB) Mhandisi Patrick Barozi,akielezea shughuli zitakazofanyika katika maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 18 wa Wahandisi unaotarajia kufanyika Septemba 2 hadi 3,2021 jijini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Wahandisi Mhandisi Ngwisa Mpembe,akizungumza na waandishi wa habari kuelekea katika Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 18 wa Wahandisi unaotarajia kufanyika Septemba 2 hadi 3,2021 jijini Dodoma.
………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
JUMLA ya Wahandisi wataalamu 630, wanatarajia kula kiapo cha utii wa taaluma yao Kitakachotumiwa na vyombo mbalimbali kuwawajibisha pale watakapo kiuka sheria na taratibu katika majukumu yao ya kiutendaji.
Hayo yamesemwa leo Agosti 31,2021 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano mkuu 18 wa Bodi ya usajili Wahandisi nchini (ERB) Prof, Bakari Mwinyiwiwa, jana jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya Wahandisi Tanzania mwaka 2021.
Prof.Mwinyiwiwa amesema kuwa kiapo hicho kitawaandaa Wahandisi hao na kuhakikisha kuwa wanawajibika vyema katika taaluma zao,maamuzi pamoja na utendaji wao wa kihandisi wa kila siku.
“Maadhimisho hayo yamepangwa kufanyika jijini hapa, kwa siku mbili jumatano na alhamisi katika ukumbi wa Jakaya Kiwete,pamoja na mambo mengine katika maadhimisho hayo jumla ya Wahandisi 630, watakula kiapo ya utii wa taaluma yao ili kuwafanya wawajibike katika utendaji wa mambo mbalimbali kwenye taaluma yao,”amesema Prof.Mwinyiwiwa
“Bodi ilianzisha utaratibu wa wahandisi wataalamu wote kula kiapo cha utii kwa taaluma yao na kwamba itakuwa ni mwiko kwao kukiuka miiko ya taaluma ya uhandisi”amesema Prof. Mwinyiwiwa
Ameongeza kuwa maudhui ya kiapo hicho yatakuwa ni wahandisi kuanza kuitumikia taaluma kama mtaalamu, kiapo kitamkumbusha jukumu lake kitaalamu na umuhimu wa kuzingatia taaluma wakati wote.
Amefafanua kuwa kiapo kitaufanya umma ujenge imani kwa Wahandisi husika,kitatumika dhidi ya muhandisi atakapo vunja miiko na maadili ya taaluma katika kumchukulia hatua Mhandisi atake kiuka kiapo chake.
“Kiapo kitamlinda Mhandisi dhidi ya kulazimishwa kutenda mambo ambayo ni kinyume na taaluma yake,pia kitamkumbusha kuzingatia thamani ya fedha,usalama wa maisha ya binadamu na mazingira,kutoruhusu masuala ya jinai,kidini,jinsia,ukabila,rangi,milengoya kisiasa katika kutekeleza kazi zake za uhandisi”amesisitiza Prof. Mwinyiwiwa
Amesema katika majadiliano kitaaluma mada kuu itakuwa ni athari za mapinduzi ya nne ya viwanda kwenye miundombinu na viwanda kwa uendelevu wa uchumi wa kati.
“Pia zitakuwepo mada ndogo kamavile mafunzo na kujenga uwezo,miundombinu na maendeleo ya viwanda, namna na mbinu za kuhimili msongo wa mawazao kwa afya njema”amesema Prof. Mwinyiwiwa
Kadhalika amesema katika maadhimisho hayo kutakuwa na zoezi utoaji wa tuzo kwa Wahandisi na wahitimu wa taasisi.
“Hii ni moja ya shughuli kubwa itakayofanyika wakati wa kuadhimisha siku ya wahandisi kwa mwaka huu bodi itatoa tuzo kwa makundi ya wahandisi wahitimu kutoka vyuo vikuu na taasisi za uhandisi nchini mwaka 2019/20″amesema
Ameeleza kuwa tuzo hiyo itakuwa ni kwa ajili ya Taasisi iliyotia fora kwenye maonyesho ya teknolojia na ubunifu,taasi iliyo tia fora kwenye maonyesho ya biashara,taasisi iliyotia fora kwenye maonyesho ya huduma za kitaaluma na taasisi iliyotia fora kwenye maonyesho ya uchuuzi.
Vilevile, amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhuduriwa na watu zaidi ya 3,500 na wengine 2,000 watashiriki kwa njia ya mtandao kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Msajili Bodi ya usajili Wahandisi nchini Patrick Barozi, amesema kuwa hadi sasa wahandisi 17, wamechukuliwa hatua za kinidhamu kwa makosa mbalimbali.