Balozi Kasyanju (kushoto) akiwa na Mkurugenzi na Mmiliki wa LIMAX Group,
Bw. Tom van WALSEM (wa kwanza kushoto); Mkurugenzi Mwendeshaji, Bw. Rob
Menheere (wa pili kushoto); na Meneja Biashara, Bw. Mark Duppen (wa tatu
kushoto) wakikamilisha mazungumzo yao baada ya zoezi la kutembelea mashamba ya uyoga
mjini Horst, Uholanzi kukamilika. —————————- UYOGA WA TANZANIA KUPATA SOKO NCHINI UHOLANZI Kampuni maarufu
ya Uholanzi, LIMAX B.V. (LimaxGroup) imedhamiria kuwekeza kwenye Sekta ya Uyoga
nchini Tanzania kwa kujenga kiwanda cha kusindika na kukausha uyoga Mkoani
Iringa kwa thamani ya Euro milioni 2.1 ambazo ni sawa na Shilingi Bilioni 5.5
za Tanzania. Hayo yameelezwa kufuatia Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe.
Irene Kasyanju kutembelea kampuni hiyo tarehe 26 Agosti 2021 na kufanya
mazungumzo na Mkurugenzi na Mmiliki wa kampuni hiyo, Bw. Tom VanWalsem. Balozi Kasyanju
alieleza kuwa uwekezaji huo utakapokamilika, Tanzania itafaidika kwa kiasi
kikubwa kutokana na mtiririko wa biashara ya uyoga kukua kwa kasi duniani
ambapo kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), biashara hiyo
inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 62.2 ifikapo mwaka
2023 kutoka Dola za Marekani bilioni 42.4 mwaka 2018. Balozi Kasyanju aliendelea kueleza kuwa Kilimo cha uyoga ni sekta inayostawi nchini Tanzania na thamani yake ya kila mwaka inakadiriwa kuwa Tsh. Bilioni 4. Hivyo, ni dhahiri kuwa uwekezaji wa LimaxGroup utakuwa na tija kubwa na wazalishaji wa uyoga nchini watafaidika na soko kubwa lililopo katika Jumuiya ya Ulaya likiongozwa na Uholanzi ikifuatiwa na Ujerumani na baadaye Poland. Balozi Kasyanju
akiwa katika kampuni hiyo alipata fursa ya kujionea mashamba ya kisasa ya uyoga
unaozalishwa (sio wa asili) na namna zao hilo lenye faida kubwa kwa binadamu linavyosindikwa
na kufungashwa (processed and packed) na kuelezea matumaini yake kuwa Tanzania
itafaidika na uwezo, uzoefu na utaalam mkubwa wa biashara wa Kampuni hiyo. “Tanzania ni nchi yenye maeneo makubwa ya misitu yenye
aina anuwai ya uyoga wa porini kwa ajili ya kula, na jamii zimekuwa zinategemea
maarifa asilia kukusanya uyoga huo kwa matumizi na kuuza katika masoko ya ndani
tu. Ni wakati muafaka sasa kufanya kazi pamoja kukuza ukuaji wa sekta hii
kibiashara”., Balozi Kasyanju alisema. LIMAXGroup itatoa mafunzo ya kuhifadhi na kuvuna uyoga wa
porini kwa madhumuni ya biashara na kulinda mazingira pia. Aidha, ujenzi wa
kiwanda hicho mkoani Iringa kutawawezesha wakulima kuuza uyoga wanaozalisha moja
kwa moja kiwandani, kuongeza ajira kwa Watanzania na kukuza mnyororo wa thamani
wa kilimo cha uyoga nchini. |