Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani akikagua nyaraka za sehemu ya vifaa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Usinge wilayani Kaliua.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani akielekea leo katika ukaguzi wa vifaa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Usinge wilayani Usinge.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Paul Matiko akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani ambaye alikuwa na ziara ya utekelezaji wa wa agizo la Waziri Mkuu alilotaka uchunguzi wa matumizi ya fedha katika Kituo cha Afya cha Usinge.
Picha na Tiganya Vincent
********************************
NA TIGANYA VINCENT
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani ametoa siku saba kwa Kamati ya Uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya wa Kaliua kutoa taarifa ya matumizi ya zaidi milioni 600 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Usinge.
Alitaka taarifa hiyo kufuatia utata kwenye maelezo ya maendeleo ya ujenzi yaliyotolewa kwa Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa ile iliyotolewa kwa Waziri Mkuu hivi karibuni wakati wa ziara yake wilayani Kaliua.
Balozi Dkt.Batilda alitoa kauli hiyo leo wakati ziara ya kikazi wilayani Kaliua ili kutekeleza la agizo la Waziri Mkuu alilotaka uchunguzi wa matumizi ya fedha katika Kituo cha Afya cha Usinge.
Alisema katika taarifa ya awali iliyotolewa na Mtendaji wa Kata ya Usinge kwa Kamati ya Usalama ya Mkoa iliyoonyesha uwepo wa akiba ya kiasi cha shilingi milioni 250 .
Balozi Dkt. Batilda alisema katika taarifa ya Kurugenzi Mtendaji kwa Waziri Mkuu ilionyesha kuwa wameshatumia kiasi cha zaidi milioni 600 na majengo bado hayajaisha.
Alisema baada ya taarifa hiyo kama kutakuwepo ma ubadhirifu wa matumizi ya fedha katika mradi huo watakaobainika watachukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Awali Mkurugenzi Mtendaji Jerry Mwaga alisema katika taarifa waliyotoa kwa Waziri Mkuu hawakuweka gharama za vifaa ambavyo vilivyokuwa kuwa katika ghala.
Alisema kuwa hali hiyo ilifanya kuonekana kuwa fedha zilizotumika ni nyingi kuliko hali halisi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Paul Matiko alisema Kamati ya Uchunguzi inahusisha Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani, Wahandisi wa Wilaya wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira(RUWASA),Wakala wa Barabara Vijijini(TARURA) na Ofisi ya UsalamaWilaya(DSO)
Wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kasim Majaliwa katika Kituo hicho hakuridhishwa na matumizi ya fedha na kazi ambayo imekwisha fanyika na kutoa miezi miwili kuhakikisha wamekamisha bila hata kuongeza fedha nje ya walizopatiwa.
Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya Jengo la Wagonjwa wa Nje(OPD), Wagonjwa wa Ndani(IPD) na Upasuaji na Jengo la Wazazi.