Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua majengo ya Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Singida na Ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Singida, ambayo yamegharimu shilingi1.314 ,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipofungua jengo la Ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Singida Agosti 30, 2021. Kutoka kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Stella Mutabihirwa, Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro na Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kufungua jengo la Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Singida Agosti 30, 2021. Kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Stella Mutabihirwa, kulia ni Mkuu wa Moa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge na wa pili kulia ni Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua jengo la Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Singida Agosti 29, 2021. Kutoka kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Stella Mutabihirwa, Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro, na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozwa na Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro (katikati) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Stella Mutabihirwa (kulia) wakati wa ufunguzi wa majengo ya Makao Makuu ya Polisi Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Singida,
Muonekano wa Jengo la Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Singida ambalo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilifungua Agosti 30, 2021.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
……………………………………………………………………………..
MAJALIWA: SERIKALI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Agosti 30, 2021 amefungua majengo ya Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida na Ofisi za Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Singida, miradi ambayo imegharimu shilingi bilion 1.314
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Waziri Mkuu amesema kuwa amefurahishwa na mradi huo ambao ujenzi wake umetumia muda mfupi na umeokoa kiasi kikubwa cha fedha za Serikali. Ameahidi kuwa serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya vyombo vya ulinzi na usalama.
“Nawapongeza sana wasimamizi wa mradi huu kwa kuhakikisha unatekelezwa vema na kuakisi thamani ya fedha za mradi yaani value for money sanjari na kukamilika kwa wakati. Tumeelezwa hapa kuwa mradi huu uliotekelezwa kwa mfumo wa nguvu kazi yaani force account, ulianza tarehe 20 Februari, 2021 na kumalizika tarehe 15 Julai 2021 na kwa gharama ya shilingi bilioni 1.3 badala ya ile ya mkandarasi ya 1.9.”
Aidha, Waziri Mkuu amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kufuata miongozo iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya kazi kwa weledi na kuboresha mifumo ya kiutendaji wa jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kushirikiana na vyombo vingine ili kuepuka ucheleweshwaji wa upelelezi wa kesi kwa lengo la kuondoa mlundikano wa mahabusu magerezani.
“Naliagiza Jeshi la polisi liendelee kuimarisha mfumo wa ulinzi na usalama kwenye ngazi ya jamii ili kujenga mfumo wa kutambua, kutoa taarifa na kuchukua hatua za awali dhidi ya vihatarishi vya ulinzi na usalama vinavyojitokeza katika maeneo yao.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Taasisi nyingine za Serikali zinazotekeleza miradi ya ujenzi ziige mfano huo. “Ujenzi wa miradi kupitia mfumo wa nguvu kazi ukisimamiwa vema tena kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo hutoa matokeo chanya.” amesema
“Nawaomba Jeshi la Polisi liendeleze ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama vya nje ya nchi pamoja na taasisi mbalimbali za kimataifa (Interpol) katika kukabiliana na kupambana na matishio ya kiusalama na makosa yanayovuka mipaka hususan ugaidi, makosa ya kimtandao (cyber-crime), uharamia, utakatishaji fedha haramu, biashara haramu ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu, ujangili na bidhaa bandia,”
Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Chilo, amesema Wizara yake iko thabiti katika kusimamia Sheria na wako tayari kuhakikisha raia wote na mali zao wanaishi kwa usalama na utulivu na kutoa wito kwa watu wote wanaopanga kufanya matendo ya kiuhalifu kuacha mara moja.
Naye, Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro amesema ujenzi huo umekamilika kwa kipindi cha miezi mitano kwa kutumia mfumo wa nguvu kazi, (Force Account) ambapo jengo hilo lina ghorofa mbili, vyumba vya ofisi 30 na kumbi mbili za mikutano.