…………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wametakiwa kuthamini rasilimali walizonazo kwa kuzitangaza ili wageni wawe na taarifa sahihi juu ya vivutio vya kitalii vilivyopo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma jana, mratibu wa mbio za sokwe (Chimpanzee Half Marathon, Bi. Beltila Kaphipa ambaye pia ni Mkurugenzi wa taasisi ya Mama Africa TZ Vision Sports, alisema sababu ya kuandaa mbio hizo ni kuwavuta watu wengi kuona maisha ya Sokwe yenye mafunzo mengi.
“Kiu yangu ni kuona utalii na vivutio vingi vilivyopo Mkoa wa Kigoma hasa Sokwe waliopo Hifadhi ya Taifa ya Gombe na Mahale Mountains, unatangazwa kwa kasi ili kuitangaza Tanzania kimataifa lakini pia kuvutia watalii,” alisema Bi. Kaphipa.
Alibainisha kuwa, mgeni rasmi katika mbio hizo zitakazofanyika Jumamosi ya Septemba 4, mwaka huu ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro.
“Mbio zitaanzia katika Uwanja wa Community Centre uliopo Mwanga, washiriki wote watapewa medali na fulana. Kujisajili ni Sh 20,000 fanya mawasiliano kwa namba hizi: 0678 799 415, 0656 262 026 au 0713 747 792, unaweza pia kufanya malipo kwa Tigopesa kupitia namba ya malipo 6652886 MAMA AFRICA TZ VISION,” alisisitiza Bi. Kaphipa.
Itakumbukwa Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika sekta ya utalii ambayo pia ndiyo sekta inayochangia fedha nyingi kwenye mapato ya nchi, hivyo kupitia michezo kunaweza kuchochea ongezeko la watalii lakini pia wananchi kujifunza masuala mbalimbali juu ya tabia za wanyamapori.