Zoezi la uhakiki wa vyama vya siasa vyenye usajili kamili linatarajiwa kuanza kesho tarehe 30 Agosti, 2021. Kwa mujibu wa barua na ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na kusainiwa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, zoezi hilo litaanza kwa kuhakiki vyama vyenye ofisi zake Jijini Dar-es-salaam. Vyama vitakavyofungua zoezi hilo ni AAFP kuanzia saa mbili asubuhi na NRA saa sita na nusu mchana.
Siku ya Jumanne zoezi hilo litaendelea kwa kuhakiki vyama vya UDP na NLD, vikifuatiwa na vyama vya UMD na ADC siku ya Jumatano ya tarehe 1 Septemba, 2021.
Siku ya Alhamisi ya tarehe 2 Septemba, 2021 vyama vya CCK na Demokrasia Makini vitafanyiwa uhakiki. Siku ya Ijumaa itakuwa zamu ya chama cha CHADEMA na UPDP.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo zoezi la uhakiki litaendelea wiki inayoanza tarehe sita kwa kuhakiki vyama vya NCCR na CHAUMA kuanzia saa mbili na nusu asubuhi. Vyama vingine vitakavyohakikiwa wiki hiyo ni pamoja na vyama vya ACT-Wazalendo, CUF, TLP, SAU, ADA TADEA na DP. Uhakiki wa Chama cha Mapinduzi (CCM) utafanyika Makao Makuu ya chama hicho mkoani Dodoma siku ya Ijumaa ya tarehe 10 Septemba, 2021.
Baada ya kuhakiki ofisi za Dar-es-salaam na Dodoma zoezi la uhakiki litahamia ofisi za Zanzibar kuanzia tarehe 13 Septemba kwa kuhakiki vyama vya AAFP na NRA. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa kila chama chenye usajili kamili kinatakiwa kuwa na ofisi pande zote mbili za Muungano.
Zoezi la uhakiki wa vyama vya siasa ni takwa la kisheria kuhakikisha vyama 19 vyenye usajili kamili vinatekeleza masharti ya usajili kama yalivyoainishwa kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa na kanuni zake.