**********************************
Na Mwandishi wetu, Hanang’
MBUNGE kupitia vyuo vikuu Dkt Pauline Nahato amekabidhi mchango wa fedha wa shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UVCCM Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara.
Dkt Nahato akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa Hanang’ Vijana Jogging Club amesema anawaunga mkono vijana wa eneo hilo kwa ujenzi wa nyumba hiyo kwa kuchangia kiasi hicho cha fedha.
“Kwa kuanzia mshikamano wetu nachangia kiasi hicho cha shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya nyumba hiyo ya mtumishi wa UVCCM Hanang’ na tutaendelea kushirikiana tena,” amesema Dkt Nahato.
Hata hivyo, ameitaka jamii ya mkoa wa Manyara, kuepukana na matukio ya unyanyasaji wa jinsia yanayotokea mara kwa mara ikiwemo ubakaji kwa watoto wa kike.
“Vijana someni kwa bidii na epukeni ngono zembe ili muweze kufikia ndoto zenu mlizojiwekea katika masomo yenu hivyo zingatieni masomo na kuachana na anasa,” amesema Dkt Nahato.
Mbunge wa vijana Taifa kupitia Mkoa wa Manyara, Asia Halamga amemshukuru Dkt Nahato kwa kuwaunga mkono vijana wa Hanang’ kwani fedha hizo zitawawezesha kupita hatua.
Asia amesema Dkt Nahato ni mbunge kupitia vyuo vikuu ila ni mzaliwa wa Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara, ameshiriki ujenzi huo baada ya kuwasilisha changamoto hiyo hivyo anamshukuru kwa kujitoa kwake kwenye nyumba hiyo.
“Nyumba ya Katibu wa UVCCM Wilaya ya Hanang’ inazidi kukamilika kwani fedha hizo zitanunulia mabati ya kisasa na kuanza kuezekwa baada ya kukamilisha kupauliwa,” amesema Asia.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ Janeth Mayanja amempongeza mbunge huyo Dkt Nahato kwa kuwaunga mkono vijana wa Hanang’ katika ujenzi huo wa nyumba ya mtumishi wao.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Jenifa Omolo amesema japokuwa yeye ni Mkurugenzi mgeni kutoka Halmashauri ya Mji wa Kibaha, atashirikiana na wananchi wa eneo hilo katika kufanikisha maendeleo.
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Hanang’ Yohane Leonce amemshukuru mbunge huyo Dkt Nahato kwa kuwapatia kiasi hicho cha shilingi milioni 1.5 ya ujenzi wa nyumba hiyo.