…………………………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inatarajia kuzindua “Jogging club” yao hivi karibuni kuunga mkono juhudi za Serikali kuwahimiza watumishi wote pamoja na wananchi kote nchini kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya zao.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha mazoezi leo Agosti 28, 2021 katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bw. Bernard Marceline amesema mazoezi hayo ni maandalizi ya uzinduzi rasmi wa Club Wizara hiyo.
“Watumishi wengi wamejitokeza kufanya mazoezi, hii ni namna bora kwa watumishi kujiandaa kuelekea uzinduzi wa jogging club yetu na kuweka miili yao kwenye utimamu na leo wameanza kufanya mazoezi kuanzia saa 12:00-2:00 asubuhi hapa uwanja wa Jamhuri” amesema Bw. Bernard.
Aidha, Wizara hiyo imeweka utaratibu wa watumishi kufanya mazoezi kila wiki mara tatu kwa wiki ambapo siku ya Jumatano watafanya mazoezi katika uwanja wa shule ya sekondari Dodoma, Ijumaa watatembea kutoka Mkao Makuu ya Wizara hiyo zilizopo Mji wa Serikali Mtumba hadi barabara kuu ya Dodoma-Dar es Salaam kuanzia saa 9:00 – 10: jioni wakati siku ya Jumamosi watafanya mazoezi kuanzia saa 12:00 – 2:00 asubuhi katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Tatu Hamza mtumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo anasema mazoezi yanasaidia kuimarisha afya na kuweka miili vizuri na yanasaidia kuimarisha mwili hatua inayowafanya kutekeleza majukumu yao vema.
Katika mazoezi hayo, watumishi wa Wizara wameungana na wananchi wa Jiji la Dodoma wakiongozwa na Jumuiya ya Wanawake Tanzania ambapo Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Taifa Dkt. Philis Nyimbi amewashukuru wananchi wa Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi kufanya mazoezi kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwahimiza wananachi kufanya mazoezi kuimarisha afya zao.
“Mazoezi ni hazina ya afya, ukifanya mazoezi utaweka afya yako vizuri na kuimarisha mfumo wako wa mwili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kujikinga na tatizo la UVIKO-19 linaloisumbua dunia sasa ili kutimiza malengo yako” amesema Dkt. Philis.
Amewahimiza wananchi kutumia siku ya Jumamosi ya mwisho ya kila mwezi kufanya mazoezi nchi nzima ili kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuwahimiza wananchi kufanya mazoezi kuboresha afya zao.
Mazoezi yanafaida nyingi kwa mwanadamu ambapo yanamfanya mtu kujisikia kuwa na afya njema, kukupa mwili nguvu hatua inayosaidia mtu kufanya kazi kwa nguvu bila kujiskia umechoka, hupunguza uzito, hunyoosha na kuimarisha misuli ya mwili, kupunguza presha, husaidia kupunguza mafuta, huimarisha mifupa ya mwili, husaidia kupunguza ugonjwa wa kisukari, huboresha usingizi na husaidia kuimarisha sehemu za viungo vya mwili.