Afisa Ushirika wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma George Bisani akisoma taarifa ya mnada wa tatu wa zao la mbaazi uliofanyika katika kijiji cha Lukumbule ambapo zaidi ya kilo milioni 1.3 zimeingizwa katika mnada huo
Baadhi ya wakulima na wananchi wa kijiji cha Lukumbule wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza jana Afisa Ushirika wa wilaya hiyo George Bisani(hayupo pichani)wakati wa mnada wa tatu wa zao la mbaazi zinazouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Picha zote na Muhidin Amri,
………………………………………………………………..
Na Muhidin Amri,Tunduru
WAKULIMA wa mbaazi katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wameendelea kuvuna fedha kufuatia kupanda kwa bei ya zao hilo kutoka shilingi 1,294 katika mnada wa kwanza hadi shilingi 1,428 mnada wa tatu.
Wakizungumza, wakati wa mnada wa tatu uliofanyika katika kijiji cha Lukumbule wilayani humo,baadhi ya wakulima wamefurahi mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umewezesha kupanda kwa bei ya mbaazi kwa kila mnada.
Hadija Mitete amesema, kabla ya zao hilo kuingizwa katika mfumo wa stakabadhi ghalani hawakuwa na manufaa yoyote licha ya kutumia nguvu kubwa katika uzalishaji kutokana na wafanyabiashara kununua mbaazi kwa bei ndogo tofauti na sasa tangu Serikali ilipoanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani.
Ameipongeza Serikali kwa kusimamia mfumo huo, ambao umewasaidia kumaliza unyonge wa muda mrefu wa kukosa soko la uhakika wa zao hilo ikilinganisha na wakulima wa mazao mengine.
Hata hivyo,amewaomba wanunuzi kulipa fedha kwa wakati ili ziwasaidie kusomesha watoto na kununua pembejeo za kilimo hususani dawa(Salphur)kwa ajili ya kupulizia korosho.
Daimu Kalambo amesema, mfumo wa stakabadhi ghalani ni nzuri kwa kuwa umeleta tija kwa wakulima kwa kupata bei kubwa ya mazao yao tofauti na soko hulia ambapo wafanyabiashara walinunua mazao kwa bei wanayopanga wao jambo lililosababisha umaskini mkubwa kwa wakulima.
Ameiomba Serikali, kuendelea kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani hata kwa mazao mengine ya biashara ikiwemo mpunga ili kuwasaidia wakulima kupata soko la uhakika na bei nzuri.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa wilaya ya Tunduru George Bisani amesema, katika mnada huo jumla ya kilo 1,324.886 zimeingizwa mnadani na wanunuzi saba walijitokeza katika mnada huo.
Bisani amesema, kampuni ya Export Trading Co Ltd imeshinda ambayo imenunua mbaazi zote kwa bei ya Sh.1,428 kwa kilo moja na kufanya jumla ya Sh. 1,891,937,208.00 kuingia katika mzunguko wa fedha katika wilaya ya Tunduru kupitia zao la mbaazi.
Amesema, mpaka sasa mwenendo wa minada ni nzuri kwa bei ya mbaazi inaendelea kupanda tokea mnada wa kwanza ambayo ilikuwa Sh 1,294 kwa kilo moja.
Kwa mujibu wa Bisani,katika mnada wa pili bei ilikuwa Sh 1,341 kwa kilo moja ikiwa ni ongezeko la Sh. 47 na katika mnada wa tatu bei imefikia Sh 1,428 sawa na ongezeko la Sh 87.
Bisani, amewashukuru wakulima wote ambao wameamua kupeleka mazao yao kwenye Vyama vya msingi ili wakutanishwe na wanunuzi wenye bei ya juu(kubwa) ambayo itahamasisha wakulima wengi zaidi kupeleka mbaazi zao kwenye vyama vya ushirika na kuongeza uzalishaji katika msimu ujao.
Amewatoa hofu wakulima juu ya kukosekana kwa vifungashio(mifuko) na kusema kuwa,tayari Serikali kupitia Chama Kikuu cha Ushirika imeshaleta kwa wingi na vinatosheleza mahitaji ya wakulima wa zao hilo.
Aidha amesema kuwa,malipo ya wakulima waliopeleka mbaazi katika mnada wa tatu wataingiziwa fedha kwenye akaunti zao ndani ya siku saba tokea siku ya mnada.
Akifunga mnada huo, Kaimu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani humo(Tamcu Ltd) Pino Chikojola, ameishukuru Serikali kwa kuwadhibiti wanunuzi na walanguzi holela wa mazao ambao wanapenda wapate faida kubwa na kumuacha mkulima akiendelea na umaskini.
Amesema, mfumo wa stakabadhi ghalani katika wilaya ya Tunduru umewezesha kupandisha uzalishaji na thamani ya mazao yao.
Amewataka wakulima kujitahidi kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara ili kutatua changamoto ya umskini kwenye kaya zao kwa kuwa Serikali imeonesha dhamira ya kuwasaidia wakulima.