Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ukarabati wa majengo ya Shule ya Sekondari ya wavulana Tabora wakati alipotembelea Shule hiyo,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ukarabati wa majengo ya Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora wakati alipotembelea Shule hiyo, Agosti 28, 2021. Kulia ni Mkuu wa Shule hiyo, Deogratias Mwambuzi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama kitabua ambacho Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisajaliwa kuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora kwa nambari 590 wakati alipokagua ukarabati wa majengo ya shule hiyo,
Muonekano wa sehemu ya bweni la Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora baada ya ukarabti uliofanywa na serikali. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ukarabati huo, Agosti 28, 2021. (Picha na Ofisi ya Wziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikari inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikiisha sekta ya elimu inapata muelekeo mpana na kutengeneza fursa kwa watoto wa kitanzania kutimiza ndoto zao za kusoma katika ngazi zote mpaka vyuo vikuu.
Amesema kuwa katika kufanikisha hilo Serikali imeendelea kuboresha miundombinu kwa shule za msingi, Sekondari pamoja na kuongeza idadi ya vyuo vikuu nchini lengo likiwa ni kuwaandaa watoto kutimiza ndoto zao.
Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumamosi, Agosti 28, 2021) alipokuwa katika muendelezo wa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo Mkoani Tabora, ambapo ametembelea Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora ambako pia amefurahishwa na matokeo ya ufaulu wa shule hizo kimkoa na kitaifa sambamba na maboresho ya miundombinu yaliyofanywa katika shule hizo kongwe.
“Mheshimiwa Rais kaleta fedha nyingi sana za sekta ya elimu, kaleta Bilioni moja, akaleta tena Milioni 500 na fedha nyingine Bilioni saba ambazo naamini zimeshafika na zitajenga madarasa 590 ikiwa ni maandalizi ya kuwapokea watoto wa kidato cha kwanza, Hii Bilioni saba ni sehemu ya Bilioni 29 ambazo zimesambazwa kwa ajili ya sekta ya afya na elimu makusanyo ambayo yametokana na miamala.”
Aidha, Waziri Mkuu amesema hivi karibuni Rais Samia, ametoa kibali cha kuajiri walimu wa masomo ya sayansi, ili kukabiliana uhaba wa walimu katika masomo ya sayansi ili kuweka uwiano sawa wa ufundishaji baina ya walimu na Wanafunzi.
“Tumefurahi sana kuona kuna Watanzania wenzetu wanajitolea tunajua wanafanya kazi, napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inalitazama suala hilo kwa umakini mkubwa na ninaiagiza Ofisi ya Rais na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha walimu hawa wanapewa kipaumbele katika ajira, wameonesha uzalendo wa hali ya juu.”
Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora, Mheshimiwa Majaliwa amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha shule zote kongwe zinakarabatiwa na kuzirudisha katika ubora na ili kuwa na mazingira rafiki ya ujifunzaji na ufundishaji.
Hali kadhalika, Waziri Mkuu ameliomba Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Tabora kuweka utaratibu na kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika shule hizo.