********************************
– Asema haridhishwi na Kasi ya Mkandarasi.
– Ataka Barabara ikamilike na kukabidhiwa kabla ya October 08 mwaka huu.
– Asema habari ya ubovu wa Barabara Makongo ifike tamati.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amemtaka Mkandarasi wa kampuni ya JASCO anaetekeleza Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Makongo kuhakikisha Mradi huo unakamikika na kukabidhiwa kabla ya October 08 mwaka huu baada ya kutoridhishwa na utendajikazi wa Mkandarasi huyo.
RC Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya ukaguzi kwenye Barabara hiyo ambapo ameonyesha kuchukizwa na tabia ya mkandarasi huyo kuonekana eneo la kazi siku pekee ambayo Viongozi wanatembelea Barabara Jambo linalosababisha kusuasua kwa Mradi huo kuleta kero na mateso kwa Wananchi.
Aidha RC Makalla amesema tayari DAWASA, TANESCO na TTCL wameondosha miundombinu yao na wananchi wote wamelipwa fidia walizokuwa wakidai hivyo haoni sababu yoyote ya mkandarasi huyo kuchelewesha Mradi.
Hata hivyo RC Makalla amewaelekeza TANROAD kuhakikisha wanamsimamia ipasavyo mkandarasi huyo ili Ujenzi wa Barabara ukamilike kwa wakati.
Barabara ya Makongo Ina urefu wa Km 4.5 na ujenzi wake unagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 8 ambapo ikikamilika inatarajiwa kurahisisha usafiri kwa Wakazi wa Makongo na kupunguza msongamano wa magari kwenye Barabara ya Bagamoyo.