Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza na Balozi wa Italia hapa nchini Mheshimiwa Marco Lambardi Ikulu jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akisalimiana na Balozi wa Italia hapa nchini Mheshimiwa Marco Lambardi alipofika kwaajili ya mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam.
……………………………………………………………………………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango hii leo agosti 21, 2021 amekutana na kufanya Mazungumzo na Balozi wa Italia hapa nchini Mheshimiwa Marco Lambardi Ikulu jijini Dar es salaam.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amemhakikishia balozi huyo kwamba Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili katika nyanja mbalimbali za maendeleo. Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi kama vile Madini, Misitu na Mifugo hivyo ni Taifa lenye utajiri wa malighafi zinazorahisisha katika uanzishaji wa viwanda.
Aidha Makamu wa Rais amesema Serikali ya Tanzania inatambua mchango wa Serikali ya Italia katika kuendeleza Elimu ya Ufundi hapa nchini na kuwasisitiza kuendelea kuwekeza zaidi katika elimu hiyo kwani elimu ya ufundi imekua na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Kwa kutambua kwamba Italia ni mwenyekiti mwenza wa mkutano mkuu wa mazingira wa umoja wa mataifa utakaofanyika mjini Glasgow, Makamu Rais amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua zote za kulinda mazingira na kufanya uhifadhi ikiwemo kuendelea kupanda miti na kulinda vyanzo vya maji hivyo ni vema mataifa yalioendelea kutambua mchango wa uhifadhi ambao umefanywa na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi hizo.
Kwa upande wake Balozi Marco Lambardi amesema Italia na Tanzania zimekua na ushirikiano wa muda mrefu na hivyo wataendelea kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo pamoja na viwanda.
Amesema tayari wapo katika kufanya makubaliano ya kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Italia hadi Zanzibar ili kuendelea kukuza sekta ya utalii hapa nchini. Aidha amesema tayari wameonesha nia ya kutoa mchango katika sekta ya afya nchini na ifikapo mwezi septemba mkwa huu, ujumbe kutoka Italia utafika kukutana na uongozi wa Wizara ya Afya ili kubaini mahitaji.
Aidha Balozi Lambardi amesema serikali ya Italia ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kutengeneza wajasiriamali wengi zaidi nchini kwa maendeleo ya taifa.