****************************
Timu ya kata ya Ibungilo ndani ya manispaa ya Ilemela imeibuka kidedea kwa kuifunga timu ya kata ya Nyamanoro magoli mawili Kwa moja ikiwa ni muendelezo wa msimu wa tatu wa mashindano ya Angeline Jimbo Cup 2021 katika hatua ya makundi mchezo ulifanyika katika uwanja wa Kona ya Bwiru.
Akizungumza mara baada ya kuisha kwa mtanange huo, Nahodha wa timu ya kata ya Ibungilo Bwana Damian Paul amesema kuwa mchezo wa leo ulikuwa mgumu mno kwao kwani wamekwisha wahi kutoka sare michezo miwili mfululizo ya kwanza katika kundi lao
‘.. Tumeshatoka sare mechi mbili zile za nyuma, Kwa namna yeyote ile leo ilikuwa tushinde ingawa bado kundi letu ni gumu kutabiri mshindi ..’ Alisema
Aidha Nahodha huyo akasisitiza kuwa msimu wa kwanza wa mashindano hayo timu yao ilifanikiwa kushika nafasi ya pili wakati msimu wa pili timu yao ilishika nafasi ya kwanza hivyo kuwataka mashabiki kuzidi kujitokeza kuiunga mkono timu yao Ili iweze kutetea ubingwa wake
Kwa upande wake Nahodha wa timu pinzani ya kata ya Nyamanoro Bwana Shaban Malegesi amefafanua kuwa licha ya kupoteza mchezo huo bado hakuna timu iliyojihakikishia kuingia hatua inayofuata kwani timu zote zinapishana alama chache dhidi ya nyengine hivyo kuwaasa wachezaji wa timu yake na mashabiki kuongeza juhudi na morali Ili waweze kufuzu hatua ya robo fainali
Akihitimisha kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula Katibu wa Mbunge huyo Ndugu Kazungu Safari Idebe ameongeza kuwa mpaka sasa mashindano yanaendelea bila kuripotiwa kwa vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani na usalama hivyo kuwaasa wachezaji na mashabiki wa michuano hiyo kuzidi kudumisha amani hiyo huku akiwasisitiza wachezaji kuonyesha vipaji vyao Ili waweze kusaidiwa ikiwemo kusajiliwa katika vilabu vikubwa vya ndani na nje ya nchi sanjari na kuwaomba kuendelea kuunga mkono Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza michezo na Mbunge wa Jimbo hilo aliyedhamiria kuifanya sekta hiyo kuwa ajira na sehemu ya kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla