………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Pwani
UJENZI wa Daraja la Wami lenye urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 unaondelea wilayani Bagamoyo mkoani Pwani unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2022.
Hayo yamesemwa na Mhandisi Mshauri wa Mradi huo Gabriel Sangusangu wakati akitoe maelezo kwa wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), waliotembelea kuona shughuli zinaendelea.
Sangusangu alisema ujenzi wa daraja hilo la kisasa ambalo litatatua changamoto daraja la awali hadi mwezi Agosti 2021 umefikia asilimia 56.
Alisema ujenzi wa daraja hilo la kisasa ambalo litakuwa na njia mbili za magari, mapoja na njia za baskeli na watembea kwa miguu umegharimu Sh. bilioni 67.7 ambazo ni fedha kutoka Serikalini ya Tanzania kwa asilimia 100.
Alisema daraja hilo ambalo linajengwa umbali wa mita 670 pembeni ya daraja la zamani lililojengwa mwaka 1959 litaweza kukoa maisha ya watu kutokana na ubora wake na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi.
“Upana wa daraja hili umezingatia sehemu ya barabara, watembea kwa miguu pamoja na vizuizi kwa ajili ya usalama hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 56 matarajio yetu ni ifikapo Septemba, 2022 tutakuwa tumekamilisha,” alisema.
Alisema ujenzi huu unajumuisha ujenzi wa barabara za maingilio ya daraja kwa pande zote mbili zenye jumla ya urefu wa kilomita 3.8 ambapo kilomita 2.1 kwa upande wa Kusini ya daraja na kilomita 1.7 kwa upande wa Kaskazini ili kuweza kuunganisha daraja jipya na barabara kuu ya Chalinze – Segera.
Sungasunga alisema Mkandarasi Power Construction Corporation Ltd kutoka China alisaini mkataba wa ujenzi wa daraja Juni 28,2018 kwa gharama ya Sh.bilioni 67.77 pamoja na kodi ya ongezeko la thamani kwa muda wa miezi 24.
Mhandisi huyo alisema kazi ya ujenzi inasimamiwa na makampuni mawili ambayo ni Ilshin ya Korea Kusini na Advanced Engineering Solutions Limited ya Tanzania kwa gharama ya shilingi bilioni 4.469.
Sungasunga alisema hadi sasa, mkandarasi amekwishaleta asilimia 95 ya mitambo na vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya kazi ya ujenz! isipokuwa vile ambavyo kazi zake itafanyika baadae.
“Ujenzi wa ofisi, maabara na nyumba tisa za makazi ya mwajiri, mhandisi mshauri umemalizika kwa asilimia 100 kama inavyotakiwe kwenye mkataba. Kazi ya wjenzi wa misingi ya nguzo za daraja imekamilika kwa asilimia 100.
Ujenzi wa kuta mbili za mwanzo na mwisho wa daraja umekamilika kwa asilimia 85, ujenzi wa nguzo namba moja na nne zenye urefu wa mita 19.6 umekamulika kwa asilima 100,” alisema.
Ujenzi wa nguzo namba mbili yenye urefu wa mita 37 umekamilika kwa asilimia 100 na ujenzi wa nguzo namba tatu umefikia mita 441, sawa na asilimia 100.
Aidha mhandisi mshauri huyo alisema kumekuwe na changamoto mbalimbali kama mabadiliko ya hali ya hewa kwa mvua ambazo hazikutarajiwa.
Aidha, alitaja changamoto nyingine kuwa ni mkandarasi kucheleweshwewa malipo yaliyochelewa ya Sh. bilioni 3.
Akizungumzia ujenzi huo Mwenyekiti wa RFB, Joseph Haule alisema mradi huo umethibitisha uwezo wa Serikali ya Tanzania kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Nadhani mmeona hapa tumeambiwa asilimia 100 ya fedha za ujenzi wa daraja hili zimetolewa na Serikali yetu hivyo niwaombe Watanzania kulitunza litakapokamilika,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema iwapo Tanzania itatumia vizuri rasilimali zake itaweza kuendeleza miradi mingi ambayo itachochea ukuaji uchumi na maendeleo.