Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dastan Lutandula akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya semina iliyoandaliwa na Wizara ya Madini, Agost 23, 2021 jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya (kushoto), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dastan Lutandula (katikati) na Katibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Angel Sanga wakifuatilia Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Madini, Agost 23, 2021 jijini Dodoma.
…………………………………………………………………….
Asteria Muhozya na Tito Mselem- Dodoma
Imeelezwa kuwa yapo Mafanikio Makubwa yaliyotokana na Ushiriki wa Watanzania katika Utoaji wa Huduma Migodini huku thamani ya manunuzi yaliyofanyika ndani ya nchi yakipanda hadi kufikia Dola Milioni 579.
Pamoja na kuwepo kwa mafanikio hayo, imeleezwa kuwa, bado ipo haja kwa Serikali kupitia Wizara ya Madini kuhakikisha inaifungamanisha ipasavyo Sekta hiyo na uanzishwaji wa viwanda vinavyozalisha malighafi kwa ajili ya kuhudumia migodi nchini.
‘’Ushiriki wa watanzania kwenye utoaji wa huduma umezidi kupanda siku hadi siku, tulikuwa tunapata takwimu hapa leo, thamani ya manunuzi ya ndani kwenye migodi mikubwa imefikia karibu Dola milioni 500 na kitu, hili ni jambo kubwa sana,’’ amesema Kitandula.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Semina kwa Wajumbe wa Kamati hiyo iliyotolewa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini Agosti 23, 2021, jijini Dodoma.
Aidha, Kitandula ametumia fursa hiyo kuzipongeza benki za ndani kwa kuanza kutoa mikopo kwa wachimbaji ikiwemo miradi mikubwa katika Sekta ya Madini na kuzitaka kuangalia namna zinavyoweza kushirikiana na benki za nje ili kuwawezesha wawekezaji katika Sekta ya madini kupata mikopo itakayowezesha kuanzishwa kwa miradi mikubwa.
Pia, Kitandula ameitaka Wizara kuendelea kuijengea uelewa kamati hiyo ili kuiwezesha kuisimamia na kuishauri ipasavyo Serikali kwa ajili ya manufaa na maendeleo na ukuaji wa Sekta ya Madini nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, ameeleza kuwa, Wizara ya Madini itafanya kila linalowezekana kuhakikisha Sekta ya Madini inakua ikiwemo kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa pamoja na kuhakikisha Wizara inafikia lengo lake la kukusanya Shilingi bilioni 650 kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.
Pia, Prof. Manya ameihaidi Kamati hiyo kuendelea kupokea maoni na kuyafanyia kazi na kuongeza kuwa, Kamati hiyo inao mchango kufuatia mafanikio yaliyotokea katika Sekta ya Madini.
‘’Mhe. Mwenyekiti tunayachukua maoni na ushauri wenu kwa umakini mkubwa kwani mmekuwa sehemu ya mafanikio ya sekta kwa kuwa yamesaidia kuweka msukumo katika utekelezaji wa majukumu yetu,’’ amesema Prof. Manya.
Awali, akiwasilisha mada ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini Tume ya Madini Venance Kasiki, ameeleza kuwa, Kanuni ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini iliyoanzishwa mnamo Mwaka 2018 na kufanyiwa marekebisho Mwaka 2019 imeongeza idadi ya watanzania kwenye migodi ikiwemo kuongezeka kwa watanzania wanaotoa huduma katika migodi mikubwa.
‘’Mhe. Mwenyekiti, pia yapo mafanikio mengine ikiwemo kuimarika kwa uwezo wa watanzania katika kutoa huduma mbalimbali na kuongezeka kwa kiwango cha manunuzi ya ndani yanayofanywa na migodi mikubwa’’ amesema Kasiki.
Mada nyingine zilizowasilishwa katika Semina hiyo ya siku moja ni pamoja na Sheria ya Madini Sura ya 123 ambayo imewasilishwa na Mwanasheria wa Tume ya Madini, Hadija Ramadhani ambaye ameieleza Kamati hiyo kuwa, Marekebisho yaliyofanyika katika Sheria ya Madini yalitoa nafasi kwa ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini na kuongeza kwamba, lengo lilikuwa ni kuweka masharti ili wananchi wanufaike na rasilimali madini badala ya rasilimali hiyo kuwa ya mwekezaji.
Mada nyingine iliyowasilishwa katika Semina hiyo ni Usimamizi na Utoaji wa Leseni za Madini ambayo imewasilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Leseni na TEHAMA Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo, ambaye ameieleza Kamati kuwa hadi kufikia mwezi Juni, 2021, jumla ya Leseni 7,968 za madini zilitolewa.
Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amechukua fursa hiyo kuwashukuru Watumishi wote wa Tume ya Madini kutokana na kujituma kwao ambako kumewezesha kufikiwa kwa mafanikio ya Sekta ya Madini.
Pia, ameipongeza Kamati hiyo kutokana na ushauri inaoutoa kwa Wizara na Tume ya Madini na kueleza kuwa, inauthamini sana.