NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chamwino Mkoani Dodoma, Deo Ndejembi amefanya ziara katika Kata ya Chamwino na kutembelea Shule ya Sekondari Chamwino ambapo amekagua ujenzi wa bwalo la chakula na kuweka jiwe la msingi kwenye Bwalo la kulia chakula.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Ndejembi ameongozana na kamati ya siasa ya wilaya ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Francis Gombo na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Gift Msuya ambapo pia wametembelea Shule ya Msingi Kambarage.
Ndejembi amesema amefanya ziara hiyo ili kuona namna ambavyo utekelezaji wa miradi hiyo ya maabara, bwalo la chakula na madarasa unavyofanyika ikiwemo kukagua thamani ya fedha iliyotumika kama inaendana na ujenzi wenyewe.
” Nimefanya ziara ya kukagua miradi ya elimu kwenye Shule ya Sekondari ya Chamwino na kukagua ujenzi wa maabara lakini pia kuweka jiwe la msingi kwenye Bwalo la chakula shuleni hapo, nimeridhishwa na kasi ya ujenzi na pia thamani ya fedha inaendana na kazi yenyewe.
Utekelezaji wa miradi hii ya elimu ni muendelezo wa ahadi tulizoahidi kipindi tunaomba kura na lengo likiwa kumaliza changamoto ya mahitaji ya elimu katika Jimbo letu ili kukuza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwenye Jimbo letu,” Amesema Ndejembi.