Wawakilishi wa wakulima wa mbaazi wa kijiji cha Semeni wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ambao majina yao hayakupatikana wakionesha sanduku lenye Barua za makampuni yaliyoomba kununua mbaazi katika mnada wa pili uliofanyika katika kijiji hicho jana ambapo zaidi ya tani 1,400 zimeuzwa.
Baadhi ya wakulima wa mbaazi katika kijiji cha Semani wilayani Tunduru, wakifuatilia mnada wa zao hilo uliofanyika jana ambapo wakulima hao wamekubali kuuza mbaazi kwa bei ya Sh.1,391 kwa kilo.
*******************************
Na Muhidin Amri,
Tunduru
CHAMA Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma(Tamcu Ltd),kimefanya mnada wa pili wa zao la mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo katika mnada huo jumla ya kilo 1,145,498 zimeuzwa.
Mnada huo umefanyika katika kijiji cha Semeni kupitia Chama cha Msingi Asema Amcos ambapo makampuni matano yamejitokeza kununua mbaazi na kampuni ya Lenic Tanzania Ltd imeshinda kununua kwa bei ya Sh.1,344 kwa kilo.
Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika(TAMCU LTD)Imani Kalembo amesema, huo ni mnada wa pili wa zao la mbaazi kufanyika katika wilaya hiyo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021.
Amesema, katika mnada huo jumla ya tani 1,042 sawa na kilo 1,145,498 zimeuzwa ambapo bei ya kilo moja ya mbaazi ni Sh 1,344.
Kalembo amesema,ni furaha kama Chama Kikuu cha Ushirika kuona bei ya mbaazi inaongezeka kila mnada kwani katika mnada wa kwanza uliofanyika katika kijiji cha Mtonya bei ilikuwa Sh 1,294,lakini katika mnada wa pili bei imefikia Sh 1,344.
Amewataka wakulima kutokubali kushawishika na wanunuzi wa kati wanaonunua mbaazi kwa bei ndogo ya Sh 800 kwa kilo ambayo haina faida, badala yake kuendelea kuuza mbaazi zao mfumo wa stakabadhi ghalani kupitia vyama vya msingi vya ushirika.
Ametoa rai kwa makampuni mbalimbali,kwenda katika wilaya hiyo kununua mbaazi ambazo zinapatikana kwa wingi na kuhakikisha wananunua kwa bei nzuri ili kuhamasisha wakulima waweze kuzalisha kwa wingi.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa wilaya ya Tunduru Georg Bisani amesema,katika minada yote miwili jumla ya kilo 1,505,849 zimeuzwa ambapo katika mnada wa kwanza zimeuzwa kilo 360,531 kwa bei ya chini ya Sh. 1,277 huku bei ya juu ilikuwa Sh.1,294.
Amesema, katika mnada wa pili uliofanyika jana katika kijiji cha Semeni jumla ya kilo 1,145,498 zimeuzwa kwa bei ya Sh.1,344 na kufanya jumla ya fedha zote zilizoingia kwenye mzunguko kutokana na minada yote miwili ya mbaazi wilayani Tunduru kuwa Sh. Bilioni 1,536,167,320.00.
Wakulima wa mbaazi katika kijiji hicho wameishukuru Serikali kwa kuliingiza zao hilo katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa umewasaidia kupata soko la uhakika na bei nzuri ikilinganishwa na siku za nyuma ambapo wafanyabiashara walinunua kwa bei ndogo kati ya Sh 250 na 300.
Wamesema, kuanzishwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa zao la mbaazi na mazao mengine ya kimkakati ikiwemo zao maarufu la korosho kumewasaidia kuwa na uhakika wa bei nzuri na kuepuka kulanguliwa na wanunuzi wa mitaani wasiokuwa na huruma kwao.
Hadija Omari(43)amesema, kama serikali itaendelea na kusimamia mpango wa kuuza mbaazi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani basi wakulima wengi watahamasika kuongeza uzalishaji na hivyo kuondokana na umaskini katika familia zao.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuhakikisha inawabana na kuwachukulia hatua kali baadhi ya wanunuzi wachache wanaopita mashambani na vijijini kuwalaghai wakulima ili wauze mbaazi kwa bei ndogo isiyolingana na gharama halisi za uzalishaji.
Mkulima mwingine Omari Misoya amesema, licha ya malipo kuchelewa mara wanapouza,lakini mfumo wa stakabadhi ghalani umesaidia kupata bei nzuri ya mbaazi wanazolima ikilinganisha na bei za walanguzi wa mitaani.
Amesema,mfumo huo umeleta heshima kubwa kwa mkulima na pia usalama wa fedha wanazolipwa kwani zinapitia moja kwa moja benki badala ya kupewa mkononi jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.
Ameitaka Serikali kupitia wizara ya kilimo kuyabana makampuni yanayonunua mbaazi kulipa fedha kwa wakulima haraka ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili kwenye familia zao ikiwemo mahitaji ya shule kwa Watoto wao.