Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifanya mazoezi ya kuimarisha afya zao yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Agnes Meena (mbele ya kamera) akizungumza kuhusu utaratibu wa mazoezi, mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI yaliyofanyika kwenye ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifanya mazoezi ya viungo kuimarisha afya zao yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
*********************************
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 21 Agosti, 2021
Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Agnes Meena amesema, Ofisi ya Rais-UTUMISHI itaendelea na utaratibu wake wa kufanya mazoezi kila Ijumaa ya wiki tangu ianze rasmi utaratibu huo tarehe 11 Agosti, 2021 kwa lengo kujenga afya za watumishi wake, ikiwa ni pamoja na kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya kurejesha michezo ya SHIMIWI kwa Watumishi wa Umma yaliyotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI yaliyofanyika kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Mkurugenzi Meena amesema kuwa, mazoezi hayo ni endelevu na hayatokuwa kwa ajili ya michezo ya SHIMIWI tu kwani yamelenga kujenga afya za watumishi ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi wanaofuata huduma katika ofisi hiyo.
Aidha, Mkurugenzi Meena amesema watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiwa mazoezini, wamefarijika sana kutembelewa na viongozi wa SHIMIWI Taifa ambapo Naibu Katibu Mkuu SHIMIWI Taifa Bw. Alex Temba amewapongeza watumishi hao kwa kuanza utaratibu wa mazoezi.
Naye, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uchambuzi na Ushauri wa Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Nolasco Kipanda amesema, mazoezi wanayoyafanya ni sehemu ya kuboresha afya zao hivyo yatasaidia kuboresha ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi wote.
“Ukiwa mtumishi wa umma na unafanya mazoezi, utafanikiwa kutekeleza wajibu wako vizuri, kwa mantiki hiyo ninashauri watumishi wa umma tuendelee kufanya mazoezi kila mara ili kuwa na afya bora,” Bw. Kipanda amehimiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Musa Magufuli amewasihi watumishi wa ofisi yake kuzingatia muda wa mazoezi uliopangwa na menejimenti ambao ni saa kumi na moja kamili jioni kila Ijumaa ya wiki.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeendelea na utaratibu wa watumishi wake kufanya mazoezi mara moja kwa wiki kwa lengo la kujenga afya za watumishi wake ili kuboresha utendaji kazi unaoendana na Kaulimbiu ya Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE.