Meneja wa KAIZEN kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bi.Jane Lyatuu akizungumza baada ya kufungua mafunzo kwa wanahabari kuhusu namna ya kutekeleza KAIZEN katika majukumu yao. Semina hiyo imetolewa leo katika Chuo Cha Biashara (CBE) Jijini Dar es Salaam.
Afisa Biashara wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw.Festo Kapela akizungumza katika mafunzo kwa wanahabari kuhusu namna ya kutekeleza KAIZEN katika majukumu yao. Semina hiyo imetolewa leo katika Chuo Cha Biashara (CBE) Jijini Dar es Salaam.
Bw.Richard Benaya akizungumza katika mafunzo kwa wanahabari kuhusu namna ya kutekeleza KAIZEN katika majukumu yao. Semina hiyo imetolewa leo katika Chuo Cha Biashara (CBE) Jijini Dar es Salaam.
Wanahabari wakifuatilia mafunzo ya KAIZEN yanayotolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara .Semina hiyo imetolewa leo katika Chuo Cha Biashara (CBE) Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
********************************
MAADHIMISHO Ya Falsafa ya KAIZEN kwa mwaka 2021 yanatarajiwa kufanyika nchini Tanzania kwa siku tatu ambapo nchi zipatazo 20 zinatarajiwa kushiriki maadhimisho hayo na kubadilishana uzoefu katika kukuza sekta ya viwanda na biashara.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari na wasanii Meneja wa KAIZEN kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bi.Jane Lyatuu amesema, kwa mwaka huu Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo yatakayofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 26 Agosti na yatafunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Tanzania bara kufungwa na Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Visiwani Zanzibar.
Amesema, nchi zipatazo 20 zitashiriki maadhimisho hayo kwa njia za mtandao huku washiriki wengine wakishiriki kwa kukutana na kueleza kuwa hiyo ni fursa kubwa kwa watanzania katika kuvutia wawekezaji, kutangaza bidhaa pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini pamoja na kuhamasisha nchi nyingine za Afrika ambazo hazijaanza kutumia falsafa ya KAIZEN kuanza kuitekeleza.
“Kupitia maadhimisho haya Tanzania inapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa nchi hizo mbinu bora za kutumia falsafa ya KAIZEN katika kukuza sekta ya viwanda na biashara nchini”. Amesema Bi.Jane.
Katika mkutano huo kutakuwa na majadilano maalum na Tanzania itapata wasaa wa kuwasilisha sera na uendelezaji wa falsafa ya KAIZEN nchini pamoja na washiriki kupata nafasi ya kutembelea viwanda na kujionea namna falsafa ya KAIZEN inavyotekelezwa.
KAIZEN ni neno la kijapani lenye maana ya ‘badilika’ kwa ubora/uzuri na hutumika katika biashara, KAIZEN huusu shughuli endelevu zinazofanyika ili kuboresha kazi, mfumo, michakato na nyanja zote za kuendesha biashara.