************************
NA MWANDISHI WETU
MSEMAJI wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba, amekemea vitendo vya baadhi ya viongozi wa dini na Wabunge wanaomtuhumu Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali chanjo, huku akivishauri vyombo vya Dola kutowafumbia macho watu hao.
Kauli hiyo ameitoa leo Agosti 20, 2021 wakati akitoa tamko la Taasisi na Jumuiya za Kiislamu kuhusu yanayoendelea nchini.
Amesema hatua ya baadhi ya viongozi wa dini na wabunge kupinga chanjo iliyoidhinishwa na serikali kwa kutoa kauli chafu dhidi ya Rais Samia na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, havipaswi kuvumiliwa.
“Tunashangazwa na matamshi ya baadhi ya viongozi wa dini hasa Askofu Josephat Gwajima, kupinga chanjo na kwenda mbali zaidi kumtuhumu Rais na Waziri kwamba wamehongwa, huku vyombo vya dola vimekaa kimya,” amesema Sheikh Katimba.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa kuhongwa ni kosa la jinai, anayezungumza hilo angepaswa kuitwa atoe ushahidi wa kisayansi kuhusu anaowatuhumu.
“Tunaishauri serikali kutomfumbia macho yeyote anayehatarisha amani ya nchi, sisi waislamu tunamuunga mkono Rais Samia na tutaendelea kutetea,” ameongeza.
Kuhusu madai ya Katiba Mpya, Sheikh Katimba, amesema kwa sababu wananchi wameanza kuona matunda ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita hapana budi kumpa muda Rais akamilishe mambo mengine ndipo afanyie kazi Katiba.
Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa hatua ya serikali chini yake kupitia muhimili wa Mahakama kuwaachia huru Masheikh 34 waliotuhumiwa kwa ugaidi.
Ameeleza kuwa mbali na kuachiwa kwa Masheikh hao, bado kuna wengine zaidi ya 300 wapo ndani na kwamba hatua mbalimbali zinafanywa kukamilisha kesi zao.
Amebainisha kuwa baadhi ya waislamu walikuwa na mtazamo hasi dhidi ya uongozi wa mwanamke, lakini utendaji wake umethibitisha utawala wa haki na sheria.
“Wengine walisema inakuaje tunaongozwa na mwanamke, tukaeleweshana kwamba hii siyo nchi ya kiislamu tukaelewana, lakini tu nafurahi tumeona matunda ya uongozi wake,” amesema Sheikh Katimba.