Hayo yamebainishwa na washiriki wa Mdahalo wa kubadilishana mawazo ili kuimarisha maarifa,Taaluma,Ujuzi na weledi kuhusu wajibu wa pamoja wa wadau wa kisiasa katika kujenga na kusimamia utekelezaji wa misingi ya mfumo wa Demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania.
Mdahalo huo wa siku tatu unaoendelea Jijini Dodoma kwa kuandaliwa na Taasisi ya Mwilimu Nyerere,chini ya Mwenyekiti wa taasisi hiyo Joseph Butiku kwa ufadhiri wa FriedrichEbert Stiftung.
Washiriki wakichangia katika mdahalo huo wamesema kuwa uvunjifu wa demokrasia unatokana na watumishi wengi wa Serikali na wateule kufanya kazi zao bila kufuata misingi ya sheria na kukiuka viapo vyao.
Shallo Mahimbo, Afisa Maendeleo ya Jamii Dodoma Jiji, akichangia katika mdahalo huo amesema kuwa tatizo kubwa la kuwepo kwa changamoto za Demokrasia ni kutokana na viongozi kutokuwa na Uzalendo wa kweli na kujikuta wanalinda maslahi binafsi au mkubwa wake aliyemteua.
Shallo akizungumzia suala la mfumo wa utekelezaji wa majukumu yake amesema kuwa bado mfumo hautekelezeki kama inavyotakiwa.
Naye Fataa Ibrahim,Kamishina wa chama cha NCCR-Mageuzi Mkoa wa Dodoma,akichangia katika mdahalo huo,amesema kuwa ili kuwa na mfumo mzuri ni lazima watumishi wawe wazalendo na wenye maadili ambayo yanaendana na misingi ya katiba ya nchi.
Naye Aisa Mushi,kutoka Taasisi ya Mwalimu Nyerere,akichangia amesema kuwa sababu kubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kutokufuata mifumo ya utawala bora inatokana na makuzi yasiyokuwa na maadili bora.
“Tunaweza kuona kuwa pamoja na kuwepo kwa mifumo bora ya kisheria lakini bado kuna watu ambao wanakiuka misingi ya haki za binadamu na wakati mwingine kutokuchukuliwa hatua za kisheria “ameeleza Aisa.
Michango hiyo ya washiriki imetokana na mada kuu juu “Kutumika kwa mifumo ya asili (jadi) ya Afrika kama nyenzo ya kukuza utawala jumuishi wa Kidemokrasia” iliyowasilishwa na mhadhiri wa Chuo cha Serikali za Mitaa -Hombolo,Paschal Seleli.