Watendaji wa Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo (KMKM) wakiwa katika zoezi la kumpandisha Nchi kavu samaki aina ya papa ikiwa ni miongoni mwa Samaki waliovuliwa na kikosi hicho kwa majaribio ndani ya bahari ya Zanzibar huko Makao Mkauu ya KMKM Kibweni Zanzibar.
Mkuu wa Doria Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo (KMKM) Kamanda Hussein Ali Makame akizungumza kuhusu Uchumi wa Buluu unavotekelezwa kwa Vitendo na kikosi hicho wakati wa makabidhiano ya samaki waliovuliwa na (KMKM) Mjini Unguja hafla iliyofanyika Makao Makuu ya KMKM Kibweni Zanzibar.
Mkuu wa Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo (KMKM) COMMODORE Azana Hassan Msingiri akimkaribisha Mtendaji mkuu Ofisi ya Rais Ikulu (Mlikulu) Mahmoud Othman mara alipofika Ofisini hapo kwaajili ya kuopokea samaki waliovuliwa na kikosi hicho kwaniaba ya Rais wa Zanzibar Huko Ofisi za (KMKM) Kibweni Zanzibar.
**************************
Na Sabiha Khamis Maelezo 20/08/2021
Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) kimeanza kutekeleza kwa vitendo azma ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi ya kuutumia vyema Uchumi wa Buluu ili kuiinua Zanzibar kiuchumi.
Katika kipindi cha majaribio Kikosi hicho kimeweza kuvua samaki wakubwa katika bahari ya Zanzibar ikiwemo aina jodari na papa ambao wamepatikana kwenye bahari kuu ya Zanzibar.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi samaki waliovuliwa na kikosi cha (KMKM) Makao Makuu ya Kikosi hicho Kibweni Mkoa wa Mjini Magharibi, Commodore Azana Hassan Msingiri amesema kikosi hicho kimejipanga katika kuimarisha upatikanaji wa samaki wakubwa kwa kutumia vifaa na uvuvi wa kisasa ili kufikia azma ya serikali ya Uchumi wa Buluu na kuinua kipato na kuleta maendeleo nchini.
Amesema Kikosi hicho kinathamini jitihada za serikali na kinauunga mkono juhudi zinzochukuliwa na Rais katika kuinua uchumi kupitia Bahari kuu kwa lengo la kuiendeleza Zanzibar kiuchumi kupitia uchumi wa bahari.
“Kikosi cha KMKM kipo mbioni kutimiza dhamira ya Rais wa Zanzibar juu ya uchumi wa buluu, hivyo tumekuwa mstari wa mbele katika kufikia malengo hayo kupitia uvuvi wa bahari kuu kwa kuvua samaki wengi” alisema Commodore Azana.
Commodore Azana ameshukuru Rais wa Zanzibar kwa kuweza kumuamini katika kutekeleza majukumu katika kikosi hicho hivyo ameahidi kufanyakazi kwa uadilifu na kuhakikisha kuwa kikosi kitakamata na kudhibiti magendo yanayoingia na kutoka nchini.
Aidha Commodore Azana ameeleza kuwa kikosi chake kimepanga kupeleka watendaji wa kikosi hicho pamoja na vifaa Kisiwani Pemba kwa ajili ya doria ya kudhibiti magendo ya karafuu katika kipindi hichi cha uchumaji wa zao hilo unaoendelea.
Nae Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais Ikulu (Mlikulu) Mahmoud Othman amekipongeza kikosi hicho kwa kazi yao kubwa wanazozifanya za kuleta maendeleo nchini kupitia uchumi wa buluu, amekitaka kikosi hcho kuongeza juhudi zao ili kuinyanyua zaidi kwa kuimarisha doria ili kuepukana magendo
Kwa upande wake Kamanda Hussein Ali Makame Mkuu wa doria KMKM amesema kikosi kinafanyakazi kwa vitendo katika kuimarisha uchumi wa buluu pamoja kuzuia magendo nchini.
Katika hafla hiyo Kauli mbiu ni “Uchumi wa Buluu unaanza na KMKM”