*******************************
Na Mariane Mariane Mgombere, Busega-Simiyu
Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Busega wamesema suala la ukusanyaji wa mapato ni kipaumbele cha kimkakati ikiwa ni sehemu ya kuongeza tija katika ukusanyaji mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani. Hayo yamesemwa na Madiwani wakati wa Baraza la Madiwani Robo ya Nne lililofanyika siku ya tarehe 20 Agosti 2021 katika ukumbi wa Silisos.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe amesema ni muhimu kutilia mkazo wa makusanyo ya ndani kwa ili kuongeza mapato ya Halmashauri. Mhe. Muniwe amesema Halmashauri haina budi kutatua changamoto za ukusanyaji mapato ili kazi ya ukusanyaji ifanyike kwa ufanisi mkubwa. “Tuhakikishe wote wanaohusika na ukusanyaji wa mapato wanalipwa kwa wakati ili kuzuia mianya ya wizi wa fedha”, aliongeza Mhe. Muniwe.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema ni vyema kuhakikisha mapato yanaongezeka na amewaomba waheshimiwa Madiwani kusaidia na kuwa na misimamo kuhusu suala la ukusanyaji wa mapato kwani wana nafasi kubwa sana katika kuijenga Wilaya. Mhe. Zakaria amesema licha ya kuwa na siku chache akiwa kama Mkuu wa Wilaya ya Busega lakini anaamini Wilaya ya Busega inaweza kukusanya mapato zaidi ya inavyofanya sasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bi. Veronica Sayore amesema anashukuru kwa mapokezi ya madiwani, na kusisitiza kwamba suala la ushirikiano ni muhimu katika kutekeleza majukumu aliyonayo ikiwemo suala la ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo vya ndani. “Hiki ni kikao changu cha kwanza cha Baraza, naamini nitapata ushirikiano kutoka kwenu, ili tuendeshe Halmashauri kwa pamoja na kusimamia majukumu yote”, aliongeza Bi. Sayore.
Aidha, Madiwani wamepongeza hatua mbalimbali zinazofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega katika suala la ukusanyaji wa mapato, na kuahidi kwamba wataonesha ushirikiano mkubwa ili kuimarisha mapato ya Halmashauri. Pamoja na hayo baraza hilo, limeweza kuazimia masuala mengine ikiwemo kufutwa kwa suala la mwekezaji aliyetaka kununua ekari 100 katika Viwanja vya Nyanza vinavyomilikiwa na Halmashauri kwa kile kinachoelezwa kutokuwa na uhakika na mwekezaji huyo.