Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Germana Leyna (wa kwanza kushoto) na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula nchini Tanzania Bi. Sarah Gordon-Gibson wakionesha mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa mwaka wa fedha 2021/2022 mara baada ya kuusaini
Baadhi ya Wataalamu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) wakishuhudia zoezi la utiaji saini wa mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kati ya TFNC na WFP
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula nchini Tanzania Bi. Sarah Gordon-Gibson (aliyevaa koti jeupe) akielekezwa namna ya kuangalia mchanganyiko uliotumika kutengenezea chakula cha nyongeza kupitia teknolojia ya QR Code wakati alipotembelea maabara za TFNC zilizopo Mikocheni jijini Dar es salaam.
********************************
Taasisi ya chakula na lishe Tanzania (TFNC) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) wamesaini mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa mwaka wa fedha 2021/2022 wenye thamani ya Shilingi milioni 575.7 sawa na USD 257,903.98 .
Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa mkataba huo leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Germana Leyna amesema kuwa TFNC na WFP wamekuwa na ushirikiano wa muda mrefu sasa tangu mwaka 2000 ambapo ufadhili wao umezidi kuongezeka mwaka hadi mwaka na kuiwezesha Taasisi katika kuendeleza harakati za kukabilana na utapiamlo hapa nchini.
“Kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2020/2021 WFP walitufadhili kufanya utafiti wa utengenezaji wa vyakula vya nyongeza kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi 59. Utafiti huu umefikia hatua nzuri ambapo tumeweza kutengeneza sampuli tano na katika hizo, sampuli mbili zimekubalika na kufanyiwa tathimini”
Dkt. Leyna amesema kuwa hivi sasa wanazifanyia uchambuzi ili kuona ipi imekubalika zaidi katika jamii na baada ya hapo wanategemea kile ambacho kimependelezwa zaidi na wanajamii na watoto watatafuta namna ya kukigawa kwa wajasiliamali kwa ajili ya kuendeleza uzalishaji kwa njia ya biashara”. amesema
Dkt. Leyna amebainisha maeneo makuu manne ya vipaumbele ambao wameingia nayo mkataba na WFP kuwa ni kusaidia masuala ya kisera, eneo la pili ni kusaidia masuala ya uratibu na usimamizi wa miradi, eneo la tatu ni kuijengea uwezo Taasisi pamoja na wadau wa lishe nchini na eneo la nne ni kusaidia katika kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya chakula na lishe.
Dkt. Leyna alimuongoza Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania Bi. Sarah Godon-Gibson kutembelea maabara za TFNC kukagua baadhi ya mashine ikiwemo mashine ya kuchakata aina ya virutubish vilivyomo kwenye chakula (NIR) iliyonunuliwa na WFP kwa gharama ya shilingi milioni 67. Baada ya kuona mashine hio Bi. Godon-Gibson alifurahishwa na ufanyajikazi wake na hivyo kuahidi kuendelea kutoa msaada kwa TFNC.
“Moja ya vipaumbele vyetu katika nchi yoyote ni kufanya kazi kwa karibu na kwa kushirikiana na Serikali, na hii ni moja ya mfano wa ushirikiano wetu na Serikali, na ikiwa tunaongeza misaada kwa TFNC tunaongeza kwa sababu tunaona wao ni washirika watu wazuri, watoa huduma kama ilivyokusudiwa, wanawajibika ipasavyo kufikia malengo”
Ameongeza kuwa “hivyo hii inatushawishi sisi kuendelea kufanya nao kazi zaidi na zaidi na ninaomba niwahakikishie kuwa tutaendelea kufaya kazi kwa kushirikiana na TFNC na kuendelea kutoa mchango wetu wa kitaalamu na kifedha. Tunathamini sana ushirikiano tuliokuwa nao na natumai tutaendelea kushirikiana” amesema Bi. Godon-Gibson.