***********************************
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dr. Dorothy Gwajima ameagiza jengo la huduma za mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, likamilike na kuanza kutoa huduma kabla ya Disemba 31, mwaka huu, wananchi waanze kunufaika.
Pia amesema wapo watu wamegeuza kila kitu mtaji wa kisiasa huku wakipotosha umma kwa kutengebeza agenda za kisiasa na wamemtengeneza Hayati John Magufuli wao wa kufikirika.
Ametoa agizo hilo jana alipokagua ujenzi wa mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2017 ambapo pia alikagua pia utoaji huduma za afya na shughuli za maendeleo ya jamii mkoani Mwanza ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake kikazi.“Hapa tulipo bajeti ilikuwa ni bilioni 10 na zaidi, zimeshatoka bilioni 9 bila matatizo kabisa, na sasa zimebaki bilioni 6 ambazo zimepitishwa kwenye Bajeti ya Serikali ya awamu ya 6 ya 2021/2022, hizo hela zinatakiwa kuanza kutumika ili zitutoke kwenye asilimia 83 twende kwenye asilimia 100 kabla ya Disemba 31 ili vitoto vile vitavyozaliwa mwaka mpya vizaliwe humu ndani” amesema Dkt. Gwajima.
Amesema, mradi huo ni mzuri sana, ni mradi mkubwa wenye gorofa sita na vitanda 261 kwa ajili ya huduma za afya ya uzazi na mtoto na zinaweza kubeba huduma za upasuaji hadi nne kwa wakati mmoja, pia una chumba maalum kwa watoto njiti na miundombinu ya utoaji wa huduma ya hewa ya oksijeni.
Aidha Dr. Gwajima amesema ili kuendelea kuishi kwa afya njema na kushuhudia maendeleo yanayofanywa na serikali, ni muhimu wananchi wakajikinga na maradhi ikiwemo kupata chanjo ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Corona, na akasisitiza kuwa hata katika nchi za Ulaya wengi waliofariki na ugonjwa huo unaoepukika wengi ni waliokataa kuchanja.
“Usipochanja utapata maambukizi ya ugonjwa wa Corona, na kuwa kwenye nafasi kubwa ya kupoteza maisha, kama wanavyokufa kwenye nchi nyingine zote za Ulaya ambao wamekataa kuchanja, tuacheni kulishwa matango pori twendeni tukachanjwe, usipochanja utakwenda kwenye oxygen kisha kaburini,” amesema Dr. Gwajima.
Amesema chanjo ya corona ni salama na hakuna miongoni mwa waliochanjwa amegeuka kuwa zombi na kuahidi kusimamia ukweli na hatakubali kulishwa matango poli na kwamba kivuli cha Magufuli kitatembea chenyewe, mengine ni agenda za watu.“Ni marufuku kuifanya chanjo ya corona kichaka cha kujificha, hao wanaotembea na kivuli cha Magufuli wana mambo yao kwani baada ya kauli yake ya kuitaka Wizara ya Afya kujiridhisha na chanjo ilianza kazi ya kujiridhisha na chanjo hizo na laiti Magufuli angejiridhisha mifumo yake ni mibovu chanjo zingine angezifuta ,”amesema Waziri huyo wa Afya.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amesema mradi huo umekamilika kwa asilimia 80 na utakuwa mwarobaini wa kupunguza vifo vya watoto wachanga na wajawazito ambapo utatoa kipaumbele cha huduma za afya kwa mama na mtoto.
Awali Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou Toure, Dr. Bahati Msaki, amemweleza Dr. Gwajima kuwa mradi huo ni ahadi ya CCM na utaboresha huduma za afya, kupunguza msongamano wa wagonjwa, vifo vya watoto wachanga na wajawazito, utakuwa na vitanda 261, vyumba viwili vya upasuaji, wodi za wajawazito na huduma zingine.
Amesema mradi huo ulioanza mwaka 2017 unaojengwa kwa gharama sh.bilioni 10.1, tayari wamepokea sh. bilioni 9.8 hivyo wanahitaji sh.bilioni 6 kuukamilisha ili wananchi waanze kupata huduma.ssdss