Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu chuoni hapo Prof.Godliving Mtui ,akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa chuo hicho kwa Waandishi wa Habari waliofika Chuoni hapo katika ziara ya kuangalia ujenzi wa Maktaba, Hosteli, ununuzi samani na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia uliofanywa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia katika chuo hicho.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu chuoni hapo Prof.Godliving Mtui (hayupo pichani) wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa chuo hicho katika ziara ya kuangalia ujenzi wa Maktaba,Hosteli, ununuzi samani na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia uliofanywa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia katika chuo hicho.
Mkurugenzi wa Milki na Huduma za Ufundi Chuoni hapo Dkt.Yazid Mwishwa,akielezea miradi inayoendelea kufanyika katika Chuo hicho.
Muonekano wa vitavu vilivyopo katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Muonekano wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kilichopokea zaidi ya shilingi bilioni 16 zilizotolewa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya ujenzi wa Maktaba, Hosteli, ununuzi samani na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia .
Muonekano wa Jengo la Maktaba katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kilichopo jijini Mbeya baada ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kujenga Maktaba mpya yenye uwezo wa kuchukua watumiaji 2500.
Muonekano wa Jengo la Hostel za wanafunzi lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 pindi utakapokalika huo ujenzi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kilichopo jijini Mbeya baada ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kutoa Fedha kwa ajili ya ujenzi huo.
…………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Mbeya
CHUO Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kimepokea zaidi ya shilingi bilioni 16 zilizotolewa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya ujenzi wa Maktaba, Hosteli, ununuzi samani na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia .
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Agosti,19,2021 Jijini Mbeya waliofika kujionea maboresho uliofanywa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia katika Chuo hicho, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu chuoni hapo Prof. Godliving Mtui amesema wanaishukuru Wizara hiyo kwa kutoa fedha hizo.
Amesema mwaka 2019 walitembelewa na aliyekuwa Rais wa Tanzania,marehemu Dkt John Magufuli ambapo aliweka jiwe la msingi la ujenzi katika mradi wa Maktaba ambayo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 2500 kwa wakati mmoja.
Amesema gharama za ujenzi wa maktaba hiyo ni zaidi ya shilingi bilioni 5 ambapo mradi huo umegawanyika katika awamu mbili.
“Hapa Must tuna bahati tulitembelewa mwaka juzi na aliyekuwa Rais Dk. John Magufuli pamoja na mambo mengine aliweka jiwe la msingi katika mradi wa Maktaba mpya ni kubwa inaweza kuwa na watumiaji 2500, kwa ukanda huu ukiacha ile cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam hakuna zaidi ya hii na Mheshimiwa Rais kuna fedha alielekeza zije.
“Kwenye Maktaba ile kuna upande wa kwanza ambao imeishakamilika na kuna samani ambazo tumeanza kuzifunga.Awamu zote mbili za ujenzi wa maktaba hiyo zimetumia shilingi bilioni tano kwa maana ya ujenzi na kuweka samani, huu ni mradi wa kujivunia” amesema Prof.Mtui
Vilevile,amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetoa shilingi bilioni 10.9 kwa ajili ya kuboresha maabara na ununuzi wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya karakana.
“Kama nilivyosema hichi chuo kilijengwa mwaka 1980 kwa hiyo miundombinu yake imeanza kuchakaa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kufanya maboresho ambapo jumla ya shilingi bilioni 10.9 tumezipata kwa ajili ya ununuzi wa vifaa,”amesema.
Amesema kwa sasa tayari wameishapata mkandarasi na kwa ajili ya kufunga vifaa hivyo ambapo amesema kuna baadhi ya vifaa vipo bandarini na vingine vipo njiani vinakuja.
“Lengo ni kuwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia chenye vifaa vya kisasa katika karakana zake katika studio zake ni kwa ajili ya usanifu na ukadiriaji,”amesema.
Pia amesema kuna mradi mwingine wa ujenzi wa Hosteli za wanafunzi ambazo zina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 ambapo amedai hayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais mara baada ya kuelezwa changamoto hiyo alipofika chuoni hapo.
“Mradi huu tunajenga majengo yetu kwa utaratibu wa ndani miradi mingi tunafanya wenyewe kwa sababu tuna uwezo,”amesema.
Vilevile, amesema wamepatiwa milioni 750 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za watumishi ambao amedai wameweza kujenga ofisi 84 kwa ajili ya watumishi hao.
“Nichukue fursa hii kuishukuru sana Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Niseme tumejenga madarasa mawili pacha kwa kutumia fedha za ndani sio tu tunategemea serikali tu hata sisi tunajenga kwa kutumia ada na ushauri wa kitaalamu tunaotoa, tunafanya vitu vya maendeleo kila jengo lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 400.
“Nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kuipa kipaumbele Must baada ya msaada huu chuo hichi kitapaa na kuwa cha Kimataifa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alikuwa na ndoto hiyo kuhudumia ukanda wa SADEC,” amesema.