Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akikata utepe kuashiria kukipokea rasmi kivuko cha MV. SENGEREMA baada ya kukamilika kwa ukarabati wake uliogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 2.2. Kivuko hicho ambacho kinatoa huduma kati ya Kigongo Wilayani Misungwi na Busisi Wilayani Sengerema kimefanyiwa ukarabati mkubwa na tayari kinaendelea kutoa huduma. Kina uwezo wa kubeba abiria 490 na magari 24 sawa na tani 170 na kimefungwa injini mpya mbili. Tukio hilo limefanyika katika kivuko cha Kigongo Busisi Mkoani Mwanza.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akikata utepe kuashiria kukipokea rasmi kivuko cha MV. TEGEMEO kutoka kwa mkandarasi Major Songoro wa kwanza kushoto ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine Transport baada ya kukamilika kwa ukarabati wake uliogharimu kiasi cha shilingi Milioni 672. Kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Kaunda Maisome na Kanoni Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema kimefanyiwa ukarabati mkubwa na kinapelekwa mara moja kuanza kutoa huduma katika eneo hilo. Tukio hilo limefanyika katika Yadi ya Songoro iliyopo Pasiansi Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza.
Picha ni kivuko cha MV. SENGEREMA baada ya kupokelewa rasmi na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, kivuko hicho ambacho kimefanyiwa ukarabati mkubwa uliogharimu shilingi bilioni 2.2 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinatoa huduma kati ya Kigongo Wilayani Misungwi na Busisi Wilayani Sengerema. Kina uwezo wa kubeba abiria 490 na magari 24 sawa na tani 170 na kimefungwa injini mpya mbili.
Picha ni kivuko cha MV. TEGEMEO baada ya kupokelewa rasmi na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, kivuko hicho ambacho kimefanyiwa ukarabati mkubwa uliogharimu shilingi Milioni 672 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinatoa huduma kati ya ya Kaunda Maisome na Kanoni Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza. Kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 85.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akikagua injini ya kivuko cha MV. SENGEREMA mara baada ya kukipokea rasmi kivuko hicho ambacho kilikuwa kikifanyiwa ukarabati mkubwa. Kivuko hicho cha tani 170 kimekarabatiwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.2, kina uwezo wa kubeba abiria 490 na magari 24 na kimefungwa injini mpya mbili.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (MWANZA)
****************************
ALFRED MGWENO (TEMESA MWANZA)
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) imekamilisha mradi wa ukarabati wa vivuko viwili vinavyotoa huduma Mkoani Mwanza kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.9.
Vivuko hivyo, MV. SENGEREMA kinachotoa huduma kati ya Kigongo Wilayani Misungwi na Busisi Wilayani Sengerema na MV. TEGEMEO kinachotoa huduma kati ya Kaunda Maisome na Kanoni Halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema, vimefanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kufikia muda wake wa kufanyiwa ukarabati ambayo imekuwa ni desturi inayofanywa na Wakala huo mara kwa mara ili kuhakikisha vivuko hivyo vinaendelea kutoa huduma bora wakati wote vikiwa katika hali ya usalama.
Akizunguma na waandishi wa habari mapema leo katika hafla fupi za kupokea vivuko hivyo zilizofanyika katika kivuko cha Kigongo Busisi mjini Mwanza ambapo kilipokelewa kivuko cha MV. SENGEREMA na Pasiansi Ilemela katika yadi ya Songoro kilipopokelewa kivuko cha MV.TEGEMEO, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, amesema kivuko cha MV. SENGEREMA kilibainika kuwa na uchakavu mkubwa zaidi na hivyo kupelekewa kutolewa kwenye maji kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa mapema iwezekanavyo.
‘‘Kivuko kilipotolewa kwenye maji ili kazi ya ukarabati ianze kilibainika kuwa na uchavu mkubwa zaidi, hivyo kupelekea kuandaa mapitio mapya (addendum) yaliyopelekea kivuko kufungwa injini mbili mpya pamoja na propulsion unit mbili mpya zilizogharimu USD 790,550.15 sawa na TZS 1,809,956,662.92. Mabadiliko ya mkataba huu yalifanya kazi ya ukarabati kuanza rasmi tarehe 22 Aprili, 2020 kwa gharama ya TZS 2,249,181,662.92‘‘. Alisema Mhandisi Maselle na kuongeza kuwa kivuko hicho kimefungwa injini mbili mpya aina ya Marine Doosan Engine Infracore zikiwa na gearbox zake ambazo uwezo wake ni Horse Power (HP) 285 kila moja.
‘’Vile vile kivuko hiki kimewekewa vifaa vya kisasa vya kukiongoza kama Radar, GPS, Magnetic Compass, vifaa vya mawasiliano (Communication Equipment) na vifaa vya uokoaji vya kutosha kwa watu wazima na watoto ambavyo ni makoti ya kujiokoa (life jackets) na maboya (life buoys)’’. Alimalizia Mtendaji Mkuu.
Aidha, mara baada ya kupokea kivuko cha MV. SENGEREMA, tukio lililofuata lilikua ni kupokea kivuko kingine cha MV. TEGEMEO, shughuli iliyofanyika katika yadi ya Songoro iliyopo Pasiansi Ilemela Mkoani Mwanza ambapo huko pia Mhandisi Maselle alipata wasaa wa kuzungumza na waandishi wa habari ambapo aliwapa taaarifa fupi kuhusu ukarabati wa kivuko hicho.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Mhandisi Maselle amesema kampuni ya kizalendo ya M/S SONGORO MARINE TRANSPORT LTD ya jijini Mwanza ilishinda zabuni ya ukarabati wa kivuko hicho kwa gharama ya Shilingi milioni 672,417,900.00 za Kitanzania ambapo ilianza kazi hiyo mara moja ili kuhakikisha wananchi wanaotegemea kivuko hicho wanakipata baada ya muda mfupi zaidi.
‘’Kivuko hiki kimefungwa injini mbili mpya aina ya Marine Doosan Engine Infracore zikiwa na gearbox zake ambazo uwezo wake ni Horse Power (HP) 300 kila moja kina uwezo wa kusail siyo chini ya 9kn. Vile vile kivuko hiki kimewekewa vifaa vya kisasa vya kukiongoza kama Radar, GPS, Magnetic Compass, vifaa vya mawasiliano (Communication equipment) na vifaa vya uokoaji vya kutosha kwa watu wazima na watoto ambavyo ni makoti ya kujiokoa (life jackets) na maboya (life buoys)’’. Alisema Mtendaji Mkuu ambapo aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya huduma za vivuko na kuahidi kuendelea kutunza vivuko hivyo kwa kuvifanyia matengenezo kama inavyotakiwa ili viweze kudumu na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Songoro, Major Songoro akizungumza katika hafla hiyo fupi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuiamini na kuipa zabuni za kutengeneza na kukarabati vivuko na kuahidi kuendelea kufanya kazi yenye viwango na ubora uliotukuka.
Kivuko cha MV. SENGEREMA kina uwezo wa kubeba abiria 490 na magari 24 sawa na tani 170, kina urefu wa mita 55, upana wa mita 10.5 na kina cha kuelea mita 1.4, wakati Kivuko MV. TEGEMEO kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 85, urefu wa mita 37, upana wa mita 10 na kina cha kuelea mita 0.75.
Fedha zote zilizotumika kukarabati vivuko hivyo zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.