**************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere ameagiza uchunguzi ufanyike juu ya shilingi milioni 5 za fedha za matumizi ya ukarabati wa madarasa ya shule ya msingi Namelock ya Kijiji Cha Orbili Kata ya Shambarai Wilayani Simanjiro.
Fedha hizo zilitolewa kupitia mfuko wa mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, kwa ajili ya ukarabati wa madarasa matano ya shule hiyo, ambayo wakazi wake ni jamii ya kifugaji.
Makongoro amesema uchunguzi ufanyike ili kubaini namna kiasi cha shilingi milioni 5 kilivyotumika katika ukarabati wa madarasa matano ya shule hiyo.
“Mimi siyo muumini wa kuweka watu ndani, nakupa mkono wa heri usiuzabe, namuagiza Mkuu wa wilaya afanye uchunguzi na taarifa nipatiwe ili tufahamu kilichotokea na endapo kukiwa na ubadhirifu tuchukue hatua,” amesema Makongoro.
Amesema ameshangazwa na madarasa hayo kutosakafiwa chini hivyo kusababisha kuwepo na vumbi hivyo kuathiri wanafunzi pindi wakisoma.
Awali, Diwani wa kata ya Shambarai, Julius Lendauwo Mamasita amesema japokuwa yeye siyo mtaalamu wa ufundi ila hakubaliani na namna fedha hizo zilizotumika kwa ajili ya kukarabati majengo hayo.
“Mwalimu mkuu hataki ushirikiano na jamii inayomzunguka akidai kuwa hawawezi kumfanya chochote, ndiyo sababu anajiamulia kila kitu anachotaka kufanya yeye mwenyewe,” amesema Mamasita.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema anasikitishwa na kitendo cha usimamizi mbovu wa ukarabati wa majengo hayo ya shule hiyo uliofanywa na mwalimu mkuu.
“Unapopewa nafasi ya kusimamia jambo unapaswa kutimiza wajibu wako ipasavyo na siyo kufanya ubabaishaji kama hiki tunachokuona hapa,” amesema Ole Sendeka.
Hata hivyo, mwalimu mkuu wa shule hiyo Peter Kaleki amesema chuki binafsi ndiyo zimesababisha achukiwe eneo hilo hivyo hajafuja fedha zozote za maradi huo.
“Fedha zilizotolewa kwa ajili ya ukarabati ni ndogo hivyo thamani ya mradi inaonekana kupitia fedha hizo japokuwa kuna baadhi ya vifaa vimebaki tulivyonunua,” amesema Kaleki.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Hassan Serera amemuhakikishia mkuu huyo wa mkoa kufanya uchunguzi kwenye shule hiyo ili kubaini thamani halisi ya gharama za ujenzi ulivyotumika.