Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza kwenye kikao cha Watendaji wa Sekta ya Ardhi na wawakilishi wa kampuni za Upangaji na Upimaji kilichofanyika Chuo cha Mipango jijini Dodoma jana.
Sehemu ya Watendaji wa sekta ya ardhi na wawakilishi wa Kampuni za Upangaji na Upimaji wakiwa katika kikao kilichofanyika Chuo cha Mipango jijini Dodoma jana.
********************************
Na Munir Shemweta, DODOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kutumia njia mbalimbali katika kuhamasisha zoezi la urasimishaji ikiwemo Taassisi za siasa ili kuongeza kasi ya utoaji hati.
Dkt Mabula alisema hayo jana katika kikao cha Watendaji wa sekta ya ardhi, kampuni za upangaji na upimaji kilichofanyika katika chuo cha Mipango jijini Dodoma.
‘’Tunahitaji kuhamasisha zoezi la urasimishaji na tunaweza kushirikisha taasisi za siasa ili zisaidie kazi hiyo’’ alisema Dkt Mabula.
Wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Tabora hivi karibuni, Dkt Mabula alitembelea ofisi ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Tabora na kuelezwa na Mwenyekiti wa chama hicho Hassan Mwakasubi kuwa, wako tayari kusaidia uhamasishaji wananchi umuhimu wa kuwa na hatimiliki ya ardhi.
Alisema, taasisi za kisiasa zinaweza kusaidia kuhamasisha wananchi kumilikishwa ardhi badala ya kuiachia serikali pekee kwa kuwa mara nyingi taasisi hizo zimekuwa karibu na wananachi.
‘’Tunapozungumzia urasimishaji isiwe suala la hiari ni vizuri tukawaeleza wamiliki faida na kipi kinawafanya wafgurahie umiliki wa ardhi’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha, aliwaambia watendaji hao waliojumuisha Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa na Wasajili wa hati na Nyaraka kuwa, ni vizuri wakati wa uandaaji hati ni lazima watendaji wa sekta ya ardhi wakawekeana malengo ili kuweza kutoa hati nyingi na kusisistiza kuwa viwanja vyote vilivyoidhinishwa ni lazima viandaliwe hati.
Mapema akizungumza na watendaji hao, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema, uhamasishaji lazima ufanyike ili wananchi wajue kama wanapaswa kuingia kwenye zoezi hilo na kuelewa umuhimu wa upatikanaji miundombinu.
Kwa mujibu wa Lukuvi kwa sasa wamiliki wa ardhi katika maeneo ya mijini ni suala la lazima na wananchi wenye nyumba au viwanja wanatakiwa kuchangamkia zoezi hilo.