Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Nzega Amosi Kanuda akimtwisha mwanafunzi ndoo ya maji alipotembelea katika shule ya Sekondari Mwanzoli kwa ajili ya kukagua mradi wa maji kutoka ziwa Viktoria
Mkurugenzi wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Nzuwasa wilaya ya Nzega mkoani Tabora Athumani Kilundumya aliyevaa shati jeupe akitoa maelezo kwa mwenyekiti wa chama cha mapinduzi ccm wilaya ya Nzega Amos Kanuda Aliyevaa suti ya kijivu wakiwa katika shule ya Sekondari Mwanzoli wakikagua mradi wa maji toka ziwa viktoria.
Na Lucas Raphael,Tabora
Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Nzega mkoani Tabora kupitia kamati ya siasa ya wilaya hiyo imempongeza mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Nzuwasa wilaya ya Nzega Athuman Kilundumya kwa kutatua kero ya maji kwa muda mfupi iliyokuwa ikiwakabili wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana kata ya Mwanzoli.
Akitoa pongezi hizo baada ya kutembelea shule hiyo ya Mwanzoli akiwa ameongozana na kamati ya siasa ya wilaya hiyo ya Nzega mwenyekiti wa ccm wilaya ya Nzega Amosi Kanuda.
Alisema juni 18,2021 kamati ya siasa wilaya ya Nzega ilifika katika shule hiyo na kukuta changamoto ya ukosefu wa maji kwa wanafunzi hali iliyolazimika kumwagiza mkurugenzi wa Nzuwasa wilaya ya Nzega kufikisha maji katika shule hiyo.
Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa kitendo cha kufikisha maji kwa wakati kumesaidia wanafunzi kutotembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji huku akisema chama cha mapinduzi lazima kimpongeze mkurugenzi huyo kwa kutekeleza agizo la chama.
Hata hivyo alitoa wito kwa wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidi kwa kuwa changamoto iliyokuwepo ya maji imetatuliwa kwa muda mfupi.
Naye mhandisi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Nzega Thereza Makungu alisema serikali kupitia wizara ya maji ilipeleka fedha katika mamlaka hiyo Sh. 188,000,000/= kwa ajili ya utekelezaji ya mradi huo ambapo gharama za mradi huo ni 390,000,000/=.
Aidha Thereza alisema mamlaka ya maji Nzega ina jumla ya kata 10 zenye mitaa 14 na vijiji 21 na jumla ya wakazi 133,000 ambapo kata ya Mwanzoli ni kata pekee ambayo ilikuwa haipati maji ya bomba kata hiyo ina vijiji vitatu ambavyo ni Mwanzoli, Kitengwe na Idudumo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Nzuwasa wilaya ya Nzega Athuman Kilundumya alisema hivi sasa wanajipanga kusambaza maji kwa wananchi wa kata hizo huku akiwahakikishia wananchi kuwa hakuna usumbufu wowote katika mamlaka hiyo kwa mwananchi yoyote anayehitaji kupelekewa huduma ya mindombinu ya maji.
Nao baadhi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo Phibi Seleli na Magdalena Mayunga wameishukuru serikali kwa kuwasogezea miundombinu ikiwemo maji, umeme, barabara huku wakimuahidi mwenyekiti wa chama kuwa watasoma kwa bidii.
Sambamba na hayo wanafunzi hao walisema kabla ya kufika maji shuleni kwao baadhi yao walikuwa wanashindwa kwenda shuleni pindi wanapokuwa katika siku zao kwa kuhofia kwenda na uchafu.
Nae mkuu wa shule hiyo Emanuel Wilson alisema shule hiyo kabla haijapata maji wanafunzi wake walikuwa wanalazimika kukatiza masomo kwa ajili ya kufuata maji umbali mrefu na kuongeza kuwa shule hiyo hivi sasa wanafunzi wake watasoma kwa bidi kwani adha hiyo imekwisha huku wakiishukuru serikali kwa kusogeza pia miundombinu ya umeme katika shule hiyo.