Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe ,akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kukagua maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na Wizara hiyo katika Chuo Kikuu Kishiriki Cha Elimu Mkwawa Mkoani Iringa.
……………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Iringa
SERIKALI imetenga kiasi cha Sh Bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya juu nchini ikiwa ni ongezeko la takribani Sh Bilioni 106 kulinganisha na kiasi cha Sh Bilioni 464 ambacho kilitolewa kwa mwaka wa masomo uliopita.
Hayo yamesemwa leo Agosti 16,2021 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe wakati wa ziara ya wandishi wa habari kukagua maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na Wizara hiyo katika Chuo Kikuu Kishiriki Cha Elimu Mkwawa Mkoani Iringa..
Prof Mdoe amesema ongezeko hilo la fedha za mkopo wa wanafunzi wa elimu ya juu ni mojawapo ya mafanikio makubwa ya serikali ya awamu ya sita katika sekta ya elimu ambapo lengo lake ni kuona kila mwanafunzi mwenye sifa ananufaika.
” Kwenye elimu tumepiga hatua kubwa ,mwaka 2015 kiasi ambacho kilitengwa kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu ni Sh Bilioni 348, mwaka 2020/21 kiasi cha Sh Bilioni 464 kilitolewa kwa wanufaika wa mkopo na sasa katika Bajeti hii mpya ya awamu ya sita kwenye mwaka wa masomo unaoanza Oktoba mwaka huu tumetenga Sh Bilioni 570 ikiwa ni ongezeko la Sh Bilioni 106 kulinganisha na mwaka jana,” Amesema Prof Mdoe.
Kwa upande mwingine Prof.Mdoe amesema kuwa dirisha la maombi ya mkopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu lililofunguliwa Julai 9 mwaka huu litakuwa wazi hadi Agosti 31 hivyo wahitaji wenye vigezo waendelee kupeleka maombi yao kwa kufuata taratibu zote ili wasikose mkopo.
”Wanafunzi wanaoomba mikopo ya kujiendeleza na masomo ya elimu ya juu wasiharakishe kujaza na kuzirudisha fomu ili kuepuka kukosea. Kuwahi kurudisha fomu haimaanishi ndio utapata mkopo sababu taarifa za waombaji wote huchakatwa ukifika mwisho wa upokeaji maombi,” amesema Prof.Mdoe
Hata hivyo ameeleza kuwa kutakuwa na madirisha matatu ya udahili la kwanza baada ya kufunguliwa Julai 15 lilifungwa Agosti 5 mwaka huu, sasa vyuo vinaendelea na taratibu zao za ndani itakapofikia Agosti 22 wawatangaze waliochaguliwa.
“Baada ya hapo dirisha la pili litafunguliwa Agosti 24 na litakuwa wazi mpaka Septemba sita ambapo kutakuwa na taratibu za ndani za kuchagua wanafunzi,” amesema.
Prof.Mdoe amewataka wanafunzi waliomba kwenye dirisha la kwanza wajithibitishe kwenda chuo wanachotaka kwani wanaweza wakawa wamechaguliwa chuo zaidi ya kimoja ili kuacha nafasi kwa wengine.
Ametaja dirisha la tatu litafunguliwa Septemba 14 hadi 20 wale ambao bado hawajafanya udahili watumie nafasi hiyo.
“Nawaomba wanafunzi waendelee kuangalia taarifa hizi zipo kwenye tovuti za Vyuo Vikuu husika, wazipitie na kufuata maelekezo,” amesisitiza.