Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akikagua nguzo yenye jina la barabara na mtaa kama vimewekwa kwa lugha ya Kiswahili na kiingereza kama mwongozo wa uwekaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi unavoelekeza kuweka vibao hivyo kwa lugha mbili za kiingereza na Kiswahili wakati wa ziara yake katika Manispaa ya Shinyanga
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akisoma kibao jina la barabara na mtaa katika moja ya nguzo zilizowekwa katika Manispaa ya Shinyanga ikiwa ni utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ambao unatekelezwa chini ya Wizara hiyo
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akionesha na kupongeza uwekaji sahihi wa nguzo zenye majina ya barabara na mitaa wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu ya Anwani za Makazi na Postikodi katika Manispaa ya Shinyanga
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akizungumza wakati akikagua miundombinu ya Anwani za Makazi na Postikodi katika Manispaa ya Shinyanga katika moja ya nguzo zinazoonesha jina la barabara na mtaa huku nguzo hiyo ikionekana kwa upande wa majina ya kiingereza.
************************************
Na Faraja Mpina, SHINYANGA
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amekagua miundombinu ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi katika Manispaa ya Shinyanga ambapo mpaka sasa utekelezaji uliofanyika kwa mujibu wa taarifa aliyopatiwa ni kusimika nguzo zenye majina ya barabara na mitaa katika kata 4 na mitaa 11 kati ya kata 17 na mitaa 55 ya manispaa hiyo
Akizungumza katika ziara yake ya kukagua miundombinu ya Anwani za Makazi na Postikodi katika Manispaa hiyo aliyoifanya jana Agosti 14, 2021 Mhandisi Kundo amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 1 na laki 1 kwa ajili ya utekelezaji wa Mfumo huo katika Manispaa ya Shinyanga kwa mwaka wa fedha 2021/2022
Ameongeza kuwa kiasi hicho cha fedha kitatumika kuweka na kusimika nguzo zinazoonesha majina ya barabara na mitaa, kuweka namba za nyumba pamoja na zoezi zima la ukusanyaji wa taarifa za makazi, majengo na huduma zinazotolewa katika majengo hayo mfano hospitali, shule, benki n.k, majina ya barabara, mitaa, majengo na kuingiza taarifa hizo kwenye programu tumizi ya simu za mkononi ya NAPA
Mhandisi Kundo amesema kuwa taarifa zote zikiingizwa kwenye programu ya NAPA kwa usahihi zitasaidia na kumuwezesha mwananchi yeyote kufika mahali popote anapohitaji kufika iwapo akiwa na anwani kamili ya eneo hilo na kuiingiza kwenye programu tumizi ya simu za mkononi ya NAPA ambayo itamuonesha ramani na barabara ya kupita itakayomfikisha katika eneo husika analotaka kufika iwe nyumba ya mtu, hoteli, hospitali au sokoni
Aidha, Naibu Waziri huyo amesisitiza Halmashauri hiyo kutenga fedha kutoka katika mapato yao ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa kuweka Miundombinu ya Mfumo huo katika Manispaa ya Shinyanga hasa katika zoezi zima la kuipa majina mitaa na barabara kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa husika ili majina yatakayopendekezwa na kuridhiwa ndio yaandikwe katika nguzo zinazoonesha majina ya barabara na mitaa ya eneo husika
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Dkt. Philemon Sengati pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kutenga fedha za kutekeleza miradi ya mawasiliano Mkoani humo na kuahidi watahakikisha wanasimamia utelelezaji wa miradi hiyo ikiwemo mradi wa usimikaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwa ufanisi mkubwa
IMETOLEWA NA: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari