Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 16,2021 katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa wakati wa ziara ya kukagua maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na Wizara hiyo katika Chuo hicho kilichopo Mkoani Iringa.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe (hayupo pichani) wakati akizungumza leo Agosti 16,2021 katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa wakati wa ziara ya kukagua maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na Wizara hiyo katika Chuo hicho kilichopo Mkoani Iringa.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe,akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari leo Agosti 16,2021 katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa mara baada ya kumaliza kukagua maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na Wizara hiyo katika Chuo hicho kilichopo Mkoani Iringa.
Muonekano wa majengo ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa mara baada ya kufanyiwa maboresho na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika Chuo hicho kilichopo Mkoani Iringa.
……………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Iringa
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe ,amesema kuwa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi unaogharimu dola za kimarekani milioni 425 ambazo ni sawa na sh bilioni 985 unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha.
Prof.Mdoe ameyasema hayo leo Agosti 16,2021 katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa ambacho ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya serikali kwenye elimu ya Juu.
Amesema Mradi huo unaanza mwaka huu wa fedha ambapo Agosti 19 mwaka huu ,Waziri wa Fedha na Mipango,Dkt.Mwigulu Nchemba atasaini makubaliano na Benki ya Dunia kwa ajili ya mradi huo.
Amesema ndani ya miaka mitano wamepata mradi mkubwa ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia ambao ni wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi
”Mradi huo utatakelezwa katika vyuo vyote vya umma pamoja na vyuo vishirikishi,Tume ya Vyuo Vikuu,Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu,mafunzo kwa wafanyakazi waliokazini”
Prof.Mdoe amesema kuwa mradi huo utasaidia ujenzi mkubwa wa miundombinu kwa asilimia kati ya 70 mpaka 80 japo kila chuo kina tengeo lake lakini kati ya asilimia hizo itaingia kwenye ukarabati au ujenzi wa miundombinu ikiwemo kumbi za mihadhara, maabara, karakana, majengo ya utawala na vinginevyo.
“Hizo fedha nyingine zinazobaki zitaingia kenye mambo ya utawala na kufundishia, kupeleka watumishi kwenye mafunzo ili tuwe na watumishi ambao wanaendana na wakati.
“Kama umeongeza miundombinu kwa kiwango kikubwa ukawafundisha wahadhiri wako vizuri na wameajiriwa wa kutoshoa ni rahisi kuongeza udahili kwa makundi yote,” amesema
BILIONI 100 KWA AJILI YA CHUO KIKUU CHA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE OF AGRICULTURE AND TECHNOLOGY
Profesa Mdoe ameongeza kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilioni 100 ni kwa ajili ya ujenzi wa Chuo kikuu cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha Kilimo na Teknolojia ambacho kipo Butiama Mkoani Mara ambapo amesema mwaka ujao kitaanza kudahili wanafunzi.
KUANZISHA PROGRAMU MPYA 290
Aidha,Naibu Katibu Mkuu huyo amesema kupitia fedha hizo pla watasomesha wahadhiri 623 pamoja na kuanzisha Programu mpya 290 ambazo zitaendelea kuboresha ubora wa elimu nchini.
“Tutasomesha wahadhiri zaidi 623 wa Shahada ya Uzamifu na 477 wa shahada ya umahiri, tutaanzisha Programu mpya 290 tutaongeza udahili wa wanafunzi lengo kuwabeba hawa wanafunzi ambao wanaongezeka,”amesema.
MIKOPO YA ELIMU YA JUU ZAIDI YA BILIONI 106 ZAONGEZEKA
Amesema ndani ya miaka mitano Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imepata mafaniko mbalimbali katika mikopo ya elimu ya juu ambapo kwa mwaka huu imeweka tengeo la shilingi bilioni 570 kutoka bilioni 464 mwaka 2015-2016 ambapo ni sawa na ongezeko la shilingi bilioni 106.
“Lakini kwa mwaka huu wa fedha kwa upande mwaka wa masomo ambao unatarajia kuanza mwezi wa 10 mwaka huu tengeo la mikopo ni shilingi bilioni 570 na tengeo hili limelenga kuhakikisha wahitaji wote napata mikopo na hii ni kati ya mafanikio awamu ya sita.
MAKUSANYO BILIONI 15.4
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema katika ukusanyaji wa mikopo ya elimu ya juu ongezeko limekuwa kubwa ambapo kwa sasa wana uwezo wa kukusanya shilingi bilioni 15.4 kwa mwezi.
“Hata katika ukusanyaji madeni ya mikopo kuna mafanukio ambapo mwaka 2015-2016 tulikusanya bilioni 28.2 fedha hizi zimeongezeka sana mpaka bilioni 184, kwa mwaka 2020-2021 hili ni ongezeko kubwa kwa sasa makusanyo ni bilioni 15.4 kwa mwezi matamanio yetu huko tuendako kile tunachokikusanya kiweze kutosheleza kwenye bajeti tunayopanga katika kutoa mikopo kwa wanafunzi,”amesema.
YASOMESHA WAHADHIRI 746 NJE YA NCHI
Amesema katika miaka mitano 2015-2020,Wizara imesomesha Wahadhiri 746 nje ya Nchi katika Shahada ya pili au tatu ambapo amedai kati ya hao waliosoma Shahada ya Uzamivu ni 552 na Shahada ya Umahiri 194.
“Wizara huwa tunatenga fedha kwa ajili ya kusomesha wahadhiri na kwa sasa tunaendelea kusomesha wahadhiri 68 na 64 ni wa Shahada ya Uzamivu na wanne ni Shahada ya Umahiri,”amesema.
Amesema Serikali inaendelea kuajiri ili kukidhi mahitaji ya Wahadhiri katika vyuo vikuu kwa kadri ya ajira na vibali vitakavyotoka.
MIUNDOMBINU KATIKA VYUO VYA SUA, MZUMBE, UDSM, MUST na ARDHI
Amesema katika mwaka wa fedha 2015-2016 mpaka 2020- 2021 kumekuwa na ukarabati mkubwa wa madarasa kumbi za mihadhara,maabara,hosteli ,ununuzi wa vifaa vya utafiti na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Ametolea Mfano katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) umefanyika ujenzi mkubwa ambapo kuna jengo la Maabara kubwa ambapo ndani yake kuna maabara nane na madarasa nane.
“Jengo lile lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 3200 kwa wakati mmoja na ndani yake kuna Ofisi saba na vyumba vya maandalizi 11 kuna stoo saba kwa ajili ya kuhifadhia kemikali ambao ni ujenzi mkubwa wenye lengo la kuondoa changamoto kwa wanafunzi kukosa maeneo ya kujifunzia au wahadhiri kufundishia,”amesema.
Vilevile ametolea mfano wa Chuo Kikuu cha Mzumbe ambapo amesema Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imeweza kujenga mabweni ya wanafunzi manne yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000.
“Mfano mwingine Chuo Kikuu cha Mzumbe pale tumeweza kujenga mabweni ya wanafunzi manne yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 na tumejenga ukumbi wa mihadhara mkubwa ambao unaweza kuchukua wanafunzi 300 kwa wakati mmoja.Tunaendelea kuboresha mazingira kwa kuweka mfumo mzuri,”amesema.
Katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam,Naibu Katibu Mkuu huyo amesema wameweza kujenga Hosteli za Magufuli pamoja na ukarabati mkubwa wa bweni namba mbili na tano ambapo kwa sasa yanauwezo wa kuchukua wanafunzi 745.
“Tumefanya ukarabati mkubwa kule kwenye Collage ya Inginiaring kwa sababu karakana zile zilijengwa miaka mingi.Tumekarabati shule ya Sayansi asilia jengo la Kemia, kituo kikubwa cha wanafunzi kinajengwa na kuna maabara wanafunzi 2500 kwa wakati mmoja ni za ykisasa,”amesema.
Pia amesema wamefanya ukarabati katika katika Chuo Kikuu cha Sayansi Mbeya kwa kujenga Maktaba ya kisasa.
Ameongeza kuwa katika Chuo Kikuu cha Ardhi na Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Dar es salaam miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati inaendelea.
Amesema Mloganzila kuna kituo cha uwahiri wa magojwa ya moyo na jengo linajengwa limekamilika kwa asilimia 95 mwaka wa masomo unaanza mwezi wa 10 wataanza masomo ule mradi ni wa kikanda,”amesema.